Poulsen apiga bao kali nje ya uwanja

Muktasari:
- Jezi ya kwanza ambayo ilikuwa ni kubwa kimwonekano ilisomeka jina lake na nyingine ilisomeka jina liitwalo Far, limeanza kutajwa kuwa huenda hilo ndilo jina la mototo huyo ajaye.
MBONGO anayeuwasha moto akiwa na klabu ya RB Leipzig ya Ujeruman, Yussuf Poulsen aliyeweka rekodi kwenye Kombe la Dunia kule Russia, yuko mbioni kupata zawadi ya mtoto kutoka kwa mpenzi wake Maria Duus.
Poulsen (24) jina lake liliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kipindi cha Kombe la Dunia kule Russia ambako aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kufunga bao kwenye michuano hiyo.
Kupitia mtandao yake ya kijamii, mshambuliaji huyo mwenye mabao 12 kwenye Bundesliga aliposti picha yenye jezi mbili zilizotundikwa za chama lake la RB Leipzig zenye namba tisa mgongoni huku zikiwa na majina mawili tofauti.
Jezi ya kwanza ambayo ilikuwa ni kubwa kimwonekano ilisomeka jina lake na nyingine ilisomeka jina liitwalo Far, limeanza kutajwa kuwa huenda hilo ndilo jina la mototo huyo ajaye.
Aina hiyo ya picha pia ilipostiwa na Maria ambaye amekuwa akienda kwenye michezo mbalimbali ya RB Leipzig kwa ajili ya kumsapoti mpenzi wake huyo ambaye msimu huu amekuwa moto wa kuotea mbali.
Kiasili Poulsen ambaye amekuwa akiichezea Timu ya Taifa la Denmark ni mtu wa Tanga na mara kadhaa amekuwa akitua nchini kwa ajili ya kuwatembelea ndugu zake.