Peter Tino Shujaa wa Stars aliyeyumba kiuchumi-2

Muktasari:
Wiki iliyopita tulianza kuyachambua maisha ya Peter Tino, nyota wa Taifa Stars, alikotokea hadi kuzichezea Pan Africa, Yanga, Majimaji na Taifa Stars aliyoiwezesha kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980.
Wiki iliyopita tulianza kuyachambua maisha ya Peter Tino, nyota wa Taifa Stars, alikotokea hadi kuzichezea Pan Africa, Yanga, Majimaji na Taifa Stars aliyoiwezesha kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980. Endelea…
Unazi na tuhuma za kupanga matokeo
Tino anasema tofauti na wakati huu kipindi hicho kuna wachezaji ambao walikuwa wanadaiwa kuzichezea timu nyingine wakati mapenzi yao yakiwa ama Yanga au Simba na hali hiyo anasema wakati fulani ilimgharimu kwani kutokana na mapenzi yake Yanga alikuwa anapata tabu kidogo kuifunga timu hiyo ya Jangwani.
“Nilikuwa naweza kuwamaliza mabeki wote na nikabaki na kipa lakini sijui inakuwaje najikuta nashindwa kuifunga Yanga,” anasema na kuongeza kuwa hilo hata baadhi ya viongozi wa klabu alizokuwa anachezea walilijua na wakati mwingine alinyimwa namba katika mechi dhidi ya Yanga.
Makocha walikuwa wanamuweka benchi hali ambayo hakuwa anajali ingawa ilikuwa inamuumiza bado hakutaka kupingana na mawazo ya wengi.
“Hata nikikosa bao kwa bahati mbaya naambiwa aaaaaaaah yule hawezi kuifunga Yanga,” anasema Tino na kuongeza kuwa zama hizi hakuna unazi kama zamani isipokuwa kuna biashara kwa maana kuwa kipindi hicho watu walikuwa wanafanya unazi kwa mapenzi yao ya moyoni kwa klabu lakini zama hizi mechi zinauzwa.
Anafafanua kwamba kwa zama hizi unajua kabisa matokeo kabla ya mechi hali ambayo anasema inachangiwa na wachezaji kutokuwa na ajira nyingine na waamuzi kugeuza filimbi ndio mtaji wao.
Tino anatoa mfano wa matokeo ya mechi ya karibuni iliyochezwa Tanga bila ya kutaja jina la timu ambayo anasema matokeo yake yalivuja kabla mechi haijachezwa.
Tino anasema kwa zama hizi klabu zinapanga matokeo na waamuzi ambao wamepoteza dira kwa kuchukulia uamuzi ndio ajira na wanataka kuishi kwa kutumia filimbi na hivyo kupindisha maamuzi kumridhisha aliyemhonga.
“Refa anaamua kufumba macho na kutoa kadi nyekundu zisizo na mashiko au hata kutoa bao na penalti wakati mwingine ili kuhalalisha bahasha aliyopewa,” anasema.
Tino anasisitiza kuwa kwa soka la namna hiyo nchi haiwezi kufika popote licha ya jitihada zinazofanywa na baadhi ya wadau.
“Kuna ukweli kuwa waamuzi wengi hawana ajira na mbaya zaidi wapo katika ratiba za mechi, wanajua mechi zao mapema hali inayotoa mwanya wa rushwa na upangaji wa matokeo,’’ anasema.
Anaongeza kuwa wakati wao miaka ya 1980 mwamuzi wa mchezo alikuwa anajulikana siku ya mkutano wa kabla ya mechi (Pre- match meeting), unaofanyika siku hiyo ya mchezo tofauti na wakati huu ambao mwamuzi anajua mechi yake wakati mwingine wiki mbili kabla.
“Mwamuzi akishajijua ndiye anayesimama katika mechi fulani kubwa kitu anachofanya ni kujipitisha kwa matajiri wa klabu na kuwakumbusha kuwa yeye ndiye atakayesimama kati hivyo wafanye maarifa vinginevyo wasije wakamlaumu,” anasema.
Tino kakumbwa na nini?
Tino anakumbuka mengi lakini zaidi ni tukio ambalo analitaja kuwa ni kilele cha mafanikio yake katika soka, tukio hilo ni la mwaka 1979 mjini Ndola, Zambia ambapo Stars iliyosheheni vipaji iliinyuka timu ya Taifa ya Zambia (KK Eleven) mabao 2-1.
Mechi hiyo imeyaacha majina ya wachezaji wa Stars katika fikra za mashabiki wa soka Zambia, mcheza sarakasi maarufu, Ramadhani Ngobariki akiwa Zambia mwaka 2000 na kujitambulisha kuwa anatoka Tanzania alijikuta akiulizwa kuhusu wachezaji wa Stars wa wakati huo.
“Hivi yule kipa (Juma Pondamali) wenu bado yupo kweli, yule ambaye alikuwa anadaka mipira kwa nyuma na vituko vingine vingi uwanjani?” anatajiwa Ngulungu, Tino na wengine, hayo ni kati ya maswali aliyoulizwa shabiki huyo wakiwamo wachezaji wengine ambao mwenyeji wake huyo hakuwa anawakumbuka sawa sawa.
Ngobariki anasema alishangaa tangu wakati huo, vipi wachezaji wa kikosi hicho kilichomliza aliyekuwa Rais wa Zambia wakati huo, Keneth Kaunda wakumbukwe.
Tino anasema hataweza kusahau katika maisha yake yote na anasisitiza kuwa kipindi hicho ndicho kilele cha mafanikio na si kwa vingine isipokuwa ni kutokana na kujiamini, ari na nguvu waliyoitumia kuiondoa Zambia iliyokuwa imekamilika kila idara.
Anawataja baadhi ya wachezaji wenzake waliounda kikosi cha kwanza siku hiyo kuwa ni Juma Pondamali, Hussein Ngulungu, Ahmed Amasha Jellah Mtagwa, Juma Mkambi, Leopald Taso Mukebezi na Ezekiel Grayson ‘Jujuma’” anasema.
“Ngulungu alikuwa kiungo ambaye sijaona mfano wake na Mukebezi alihodhi namba katika timu ya Taifa kwa kipindi kirefu na upande wa Zambia anawakumbuka Fred Mitti, Dickson Makwaza, Dick Chama na wengine,” anasema na kuongeza kuwa Zambia walinyukwa mbele ya Rais wao, ambaye alikuwa anatoa kila kinachohitajika kwa timu hiyo.
Tino anasema kufungwa bao la kwanza ugenini hakukuwakatisha tamaa na badala yake walizidisha kasi ya mchezo na bao hilo kusawazishwa na kiungo mkabaji, Mohamed Rishard Adolf.
“Kipindi cha lala salama kona ya Mukebezi ilinikuta nimeruka huku nimebanwa na mabeki wa Zambia wapatao watatu lakini nilijivuta zaidi hewani na kupiga mpira kichwa ambao kipa wa Zambia, Kapambe Mabengwa alishindwa kuuzuia” anasema Tino huku akitabasamu kabla ya kucheka.
Anasema ushindi huo uliwawezesha kufuzu fainali nchini Nigeria lakini waliing’oka mapema katika fainali hizo baada ya kuzidiwa kiuwezo uwanjani na wenzao wa Kundi A lililokuwa na timu za Ivory Coast, Misri na wenyeji Nigeria kwa anachodai kwamba wenzao walikuwa wamepiga hatua zaidi na tayari walikuwa na wachezaji kutoka Ulaya.
Anabainisha kuwa soka lao la hiyari ya moyo halikuweza kuleta matokeo tarajiwa katika michuano hiyo hali iliyowafanya wafunge virago mapema.
Zaidi ya hilo, Tino anasema kwamba haoni ndoto za karibuni za Stars kufikia walipofikia wakati huo kutokana na kile anachodai kuwa misingi ya soka inakosekana.
Itaendelea Jumanne ijayo…