Pearl of Africa Prince Nyerere, Nasser watua kwa Museven

Muktasari:
- Tayari madereva kutoka Rwanda, Kenya, Ethiopia, Tanzania na wenyeji Uganda wameanza kuwasili mjini Mbarara, kwa ajili ya mbio hizo zinazoanza Mei 8 hadi 11, zikipewa jina la Shell V Power Pearl of Africa Rally 2025.
WATANZANIA Prince Charles Nyerere na Yassin Nasser wanatarajiwa kushiriki katika mbio za magari zitakazofanyika Mbarara, Uganda kusaka ubingwa wa Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kuchezwa Magharibi mwa Uganda, karibu na eneo ambalo Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museven anatokea.
Tayari madereva kutoka Rwanda, Kenya, Ethiopia, Tanzania na wenyeji Uganda wameanza kuwasili mjini Mbarara, kwa ajili ya mbio hizo zinazoanza Mei 8 hadi 11, zikipewa jina la Shell V Power Pearl of Africa Rally 2025.
Nasser ndiye Mtanzania aliye juu katika orodha ya madereva watakaoanza na ataondoka wa pili akitumia gari aina ya Ford Fiesta R5 akiongozwa na msoma ramani Mganda, Ally Katumba, huku Prince Charles Nyerere ataondoka wa 10 akiendesha gari aina ya Mitsubishi Evolution X.
Mkenya Karan Patel, akitumia gari aina ya Skoda Fabia ataondoka wa kwanza kutokana na orodha ya uanzaji wa madereva iliyotolewa mwishoni mwa juma na waandaaji, Shirikisho la Mbio za Magari Uganda (FMU).
Mashindano haya yataanza rasmi Alhamisi kwa zoezi la uhakiki wa njia (route reconnaissance) kabla ya zoezi la ukagauzi wa usalama wa magari (scrutineering) na kisha madereva kushiriki mbio za kupimwa uwezo (Super Special Stage).
Raundi ya pili pia imepata baraka za udhamini wa KCB Uganda ambao wamemwaga Sh80 milioni za Uganda sawa na Sh59 milioni za Tanzania.
Rais wa Shirikisho la mbio za magari Uganda, Jimmy James Akena, amewashukuru KCB kwa kuunga mkono maendeleo ya mchezo huo Afrika mashariki.
“Tunaamini mchango wa KCB utazifanya mbio hizi mjini Mbarara kuwa salama na zenye msisimko mkubwa,” alisema Rais wa FMU.
Kwa mujibu wa ratiba, mashindano yataanza kwa mbio za kufuzu (qualifying shakedown) Mei 8 kabla ya mbio rasmi kuanza Ijumaa na zitapigwa raundi tatu katika eneo la Rukaari Resort.
Raundi nyingine zitapigwa Jumamosi na Jumapili na mashindano yatamalizika rasmi na washindi kutangazwa.