Prime
Dabi ya simu inakaribia kuwakutanisha Mpanzu na Pacome

Muktasari:
- Simu nyingine tena ikawaita watu wa Yanga na Simba kwenda Dodoma. Hakutakuwa na simu nyingine yoyote kuanzia sasa mpaka kesho? Sidhani.
SIMU moja ilivunja dabi ya Yanga na Simba Machi 8. Alikiri hadharani aliyekuwa bosi mtendaji wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo wakati alipokutana na watu wa Yanga akijaribu kuwashawishi wacheze pambano la Juni 15.
Simu nyingine tena ikawaita watu wa Yanga na Simba kwenda Dodoma. Hakutakuwa na simu nyingine yoyote kuanzia sasa mpaka kesho? Sidhani.
Na sasa tuseme kwamba tuna dabi ya kukumbukwa mkononi. Dabi ambayo imewaondoa katika nafasi zao Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, mzee Steven Mnguto. Dabi ambayo imemuondoa madarakani kwa muda mtendaji wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo.
Dabi ambayo imeuweka pagumu uchaguzi wa TFF. Rais wa mpira, Wallace Karia ana wakati mgumu kwa sasa. Hii nayo inachangiwa zaidi na matokeo ya kutofanyika kwa pambano hili. Kama ikichezwa itakuwa ni Dabi ya kukumbukwa.
Nje ya uwanja hakuna ambaye ameshinda. Na-washangaa baadhi ya watu wa Simba ambao wanaonekana kutolitaka pambano kwa sababu matakwa ya Yanga yametimizwa. Ukweli ni kwamba hata matakwa ya Simba yalitimizwa Machi 8.
Yanga wamesawazisha tu kwa matakwa yao kutimizwa Juni 15. Pambano la kesho likichezwa basi hakuna mwamba kati yao. Huyu hakutaka mechi ya Machi 8, yule hakutaka mechi ya Juni 15. Ngoma droo.

Mambo ya kuangaliwa sasa yapo ndani ya uwanja. Simba inahitaji ushindi wakati Yanga inahitaji sare. Atakayepata matokeo yoyote kati ya haya anakwenda kutangazwa kuwa bingwa.
Lolote linaweza kutokea uwanjani. Yanga inaonekana kuwa na timu bora lakini Simba imepunguza pengo kubwa baina yake na Yanga kuanzia kufungwa mabao 5-1 jioni ile kwenye uwanja wa taifa, hadi kufungwa bao la kujifunga la Kevin Kijili katika pambano la raundi ya kwanza.
Kuanzia jioni ile waliyofungwa mabao matano kisha yakaanza kupungua kila walipokutana, Simba imejitahidi kubadilisha timu yake kiasi kwamba ilicheza fainali za Shirikisho dhidi ya Berkane ya Morocco. Sioni sababu yoyote ya Simba kuwa na hofu na mechi hii.
Kuna Ellie Mpanzu ambaye amekuja kuitia timu moto na ni mchezaji ambaye anaweza kubadilisha taswira ya mechi yenyewe akitumia uwezo wake binafsi ambao unakuwa mwiba kwa wachezaji wengi wa timu pinzani wanaokabiliana na Simba.

Kuna Kibu Dennis ambaye amejizoesha kuzisalimia nyavu za Yanga kila wakati. Kibu pia ni mchezaji wa mechi kubwa. Simba wanamuimba zaidi Mpanzu lakini Kibu ndiye mchezaji ambaye anaibeba zaidi timu katika mechi kubwa kwa misimu mitatu sasa.
Jean Charles Ahoua haonekani sana uwanjani lakini anakuwepo katika matukio hasa tukio la kushangilia mabao ambayo amefunga au ameyapika. Mechi yake nyingine ya Dabi baada ya kufeli katika lile pambano la kwanza. Ana jambo la kuonyesha.
Yanga ina kila mtu ambaye inapaswa kuwa naye kwa sasa. Namna ambavyo wameitengeza timu yao hauwezi kuamini kwamba wamemuuza Aziz Ki kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na bado hawana hofu yoyote ya kushinda mechi ya soka.
Prince Dube ameumia na huenda asicheze pambano hilo lakini haiwatii hofu Yanga kwa sababu mara zote akiwepo wamekuwa wakianzisha washambuliaji wawili uwanjani. Yeye na Clement Mzize. Ina maana pambano hili la mwisho la msimu wa ligi anaweza kuanza mshambuliaji mmoja kama ilivyo kwa mifumo ya timu nyingine duniani.

Mzize akumbuke tu kwamba wakati huu inapotajwa anakaribia kuuzwa na Yanga kwenda nje, ukweli ni kwamba atakuwa hajaacha kumbukumbu yoyote kwa mashabiki wa Yanga kuhusu kuziona nyavu za Simba. Hajawahi kuifunga Simba.
Wakati Pacome Zouazoua akionekana kuwa kiungo hatari zaidi kwa Yanga, mchezaji ambaye Simba wanapaswa kumuhofia zaidi ni Maxi Nzingeli. Huyu naye ni kama Kibu tu linapokuja suala la bahati ya kumfunga mtani.
Hata hivyo, Maxi sio bahati tu. Ni mchezaji wa kuchungwa hasa kwa sababu licha ya kuwa na kipaji lakini hakitegemei sana kipaji chake. Anategemea zaidi uwajibikaji wake.
Mengine tunawaachia makocha. Hata hivyo, Fadlu Davids bado ana kazi ya kufanya kuifunga Yanga hasa katika kipindi cha pili. Pumzi za Simba zinashuka kidogo kama tulivyoona katika pambano la marudiano dhidi ya Berkane.
Mengineyo? Tunataka kuona mchezaji akivunja rekodi ya mwaka 1977 iliyowekwa na Abdallah King Kibadeni wa Simba. Anabakia kuwa mchezaji pekee kufunga ‘hat trick’ katika pambano hili. Imechosha kuisikia rekodi hii kila uchao wakati kwa wenzetu katika mechi hizi kubwa wachezaji kibao wanafunga ‘hat trick’.

Jingine? Clatous Chota Chama atacheza pambano hili kwa ajili pia ya kuamua hatima yake ya kisoka hapa nchini. Msimu wake wa kwanza na Yanga amechukuliwa poa sana lakini ghafla anaweza kubadili kila kitu baada ya kesho jioni.
Haionekani kama Yanga imeweka kipaumbele sana kumuongezea mkataba mpya, na wala haionekani kama timu yake ya zamani imepania kumrudisha. Hata hivyo, ghafla kila kitu kinaweza kubadilika ikifika kesho usiku kama kuna maajabu atakayoyaonyesha kama tulivyomzoea zamani.
Mwamuzi? Filimbi aichukue Ahmed Arajiga tu. Ndiye mwamuzi anayeweza kunyoosha sheria zote na mshindi akashinda zake kihalali. Kuna kuna kadi nyekundu ya dakika ya tatu itolewe. Kama kuna penalti ya dakika ya mwisho wakati pambano likiwa bila bila basi nayo itolewe. Hakuna sheria maalumu kwa ajili ya Dabi. Sheria ni zilezile tu za soka kwa ajili ya mechi zote.