Miloud: Tupo siriazi, tunataka ushindi

Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa kabla ya mechi, Miloud amesema timu yake baada ya kuahirishwa mara mbili kwa mchezo huo haikutoka mchezoni kwani waliendelea na maandalizi.
Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud amesema kesho timu yake ipo tayari kwa mechi hiyo kubwa na kwamba wako siriazi ili kushinda mchezo huo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa kabla ya mechi, Miloud amesema timu yake baada ya kuahirishwa mara mbili kwa mchezo huo haikutoka mchezoni kwani waliendelea na maandalizi.
Mchezo huo wa dabi uliahirishwa na Bodi ya Ligi kupigwa Machi 8 na Juni 15, mwaka huu, ambapo ulisogezwa mbele hadi Juni 25.
Kocha huyo ambaye atasimamia mechi yake ya kwanza dhidi ya Simba, amesema kikosi chake kinaiheshimu Simba na kwamba umuhimu wa mechi hiyo hawatacheza kama timu ndogo kwa kupaki basi, badala yake watashambulia kwa nidhamu.
"Sisi Yanga tupo tayari kwa mchezo. Tumekuwa kwenye maandalizi kwa muda mrefu. Kulikuwa na kuahirishwa kwa ratiba ya mchezo huu, lakini tuliendelea na maandalizi tulijua kwamba kuna siku utachezwa," amesema.
"Nafahamu kwamba tunahitaji matokeo ya aina mbili kushinda na kutoa sare ili tuchukue ubingwa. Hii ni mechi ya kuamua nani bingwa, lakini najua hata Simba nao wana uhitaji wa matokeo ya aina moja tu kushinda ili wawe mabingwa.
"Yanga ni timu kubwa hatuwezi kucheza mechi kama hii kwa kukaa nyuma. Tutashambulia kutengeneza ushindi wetu, lakini tunajua kwamba tutatakiwa kuwa makini kwenye ulinzi, tunaiheshimu Simba ni timu nzuri."