Panga pangua ya Mbelgiji Sven Simba SC yamshtua January Makamba

Muktasari:
Ugeni wa kocha wa Simba, Vanderbroek unaweza pia ukawa sababu ya kubadili kikosi katika mechi tofauti ili kuwajua wachezaji wake.
Dar es Salaam.Ni kama homa ya pambano la watani wa jadi imeanza kupanda baada ya kocha wa Simba, Sven Vanderbroek kupangua kikosi chake katika mechi mbili mfululizo ili kuwapiga changa la macho wapinzani wake wakubwa Yanga atakaokutana nao Januari 4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha huyo mpya amebadilisha wachezaji nane katika kikosi cha leo kitakachoanza dhidi ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaoanza saa 10:00 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo uliopita dhidi ya Lipuli kocha huyo aliwaanzisha kipa Beno Kakolanya, mabeki Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Traone Santos, viungo Jonas Mkude, Shariff Shiboub, Clatous Chama na Fransis Kahata lakini katika mchezo wa leo wachezaji hao wote hao wameanzia benchi kasoron Kapombe ambaye hayupo kabisa.
Mbelgiji huyo amewaanzia Manula, Haruna Shamte, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Kennedy Juma, Gerson Fraga, Deogratius Kanda, Ibrahim Ajib na Mzamiru Yassin badala ya wachezaji hao walioanzia benchi.
Mabadiliko makubwa ya kikosi yalimfanya Mbunge wa Bumbuli na mwanachama wa Simba, January Makamba@JMakamba kupitia akaunti yake ya tweet kuandika: Mabadiliko makubwa ya kikosi cha kocha mpya wa @SimbaSCTanzania. Ni wachezaji watatu walioanza mechi iliyopita ndiyo wameanza (Kagere, Dilunga na Wawa). Wengine wawili (Kapombe, aliyekuwa nahodha mechi iliyopita, na Mkude) hawapo hata benchi leo. Shamte, ambaye hakuwa benchi ameanza leo.
Hali hiyo inaonyesha ni jinsi gani homa ya pambano la watani wa jadi imeanza kuwa juu kwani makoccha hata viongozi wamekuwa wakiogopa kuwaanisha baadhi ya wachezaji ili kuwalinda na kupata kadi au majeruhi yatakayosababisha wakaukosa mchezo huo mkubwa unaosubiriwa kwa hamu na watu wengi.
Hata hivyo pia ugeni wa kocha wa Simba, Vanderbroek unaweza pia ukawa sababu ya kubadili kikosi katika mechi tofauti ili kuwajua wachezaji wake.