Pacome afunguka sababu za kuitaka Simba

Muktasari:

  • Pacome amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Yanga, lakini amekuwa nje tangu alipoumia katika mechi dhidi ya Azam alipotolewa dakika 28 ya kipindi cha kwanza.

KIUNGO wa Yanga Pacome Zouzoua afunguka sababu zilizomfanya amuombe kocha wake Miguel Gamondi, kucheza katika mechi ya dabi iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Pacome amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Yanga, lakini amekuwa nje tangu alipoumia katika mechi dhidi ya Azam alipotolewa dakika 28 ya kipindi cha kwanza.

Katika mechi ya kwanza ya ligi Yanga ilipokutana na Simba na kushinda mabao 5-1, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga akiwa ametia nyavuni bao la mwisho kwa timu yake  dakika ya 86.

Akizungumza na Mwanaspoti alieleza sababu za yeye kumuomba kocha wake kucheza licha ya majeraha aliyonayo na alisema kuwa, alitamani kucheza na kusaidia timu yake bila kujali anapitia changamoto gani.

Pacome alieleza kuwa alikuwa anaumia kuona mashabiki wa Yanga wanatamani kumuona anarejea uwanjani ili aisaidie timu yao hiyo kwenye mchezo huo mgum,u

Aidha alisema,amekosa mechi nyingi muhimu jambo ambalo linamkosesha amani na kumfanya apoteze rekodi yake nzuri iliyowekwa kutokana na michezo ya aina hiyo.

"Najua mashabiki wanatamani kuniona uwanjani lakini mimi mwenyewe natamani kurejea kuitetea timu yangu, ile ni mechi kubwa na yenye presha kubwa hivyo kwangu haikuwa rahisi kuona naendelea kukaa nje,"alisema Pacome ambaye ni kiungo wa zamani wa ASEC Mimosas.

"Kocha alikataa na kuniambia nijipe muda zaidi nipone sawasawa kwani wapo wenzangu watafanya vizuri, nilikubali na kumuelewa kocha ingawa roho ilikuwa inaniuma ila kikubwa tumepata ushindi," alisema Pacome.

Yanga bado ipo kileleni katika msimamo wa ligi kwa kuwa na alama 58,katika mechi 22 walizocheza  huku wakifunga mechi 19,sare moja na kufungwa mechi mbili.