Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ouma: Wale Simba waje tu!

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo iliyopigwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, Singida ilishinda kwa mabao 3-2 yaliyofungwa na Elvis Rupia, Jonathan Sowah na Arthur Bada, huku yale ya Yanga yakifungwa na Prince Dube na Denis Nkane.

KOCHA wa Singida Black Stars raia wa Kenya, David Ouma amesema mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga imewapa morali wachezaji wakati huu wakijiandaa kucheza na Simba katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Katika mechi hiyo iliyopigwa Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, Singida ilishinda kwa mabao 3-2 yaliyofungwa na Elvis Rupia, Jonathan Sowah na Arthur Bada, huku yale ya Yanga yakifungwa na Prince Dube na Denis Nkane.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema kwa sasa wachezaji wote wako katika hali nzuri na utimamu wa kimwili, na wapo tayari kucheza na Simba katika mechi hizo muhimu zijazo, licha ya kukiri ugumu uliopo kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Tunakwenda kucheza mechi mbili mfululizo na Simba ambazo kwetu tunazichukua kwa umuhimu mkubwa sana. Malengo yetu makubwa yalikuwa ni kupata tiketi ya CAF ambayo tayari tumefanikiwa sasa kilichobaki ni kuendeleza heshima yetu,” alisema.

Kocha huyo alisema licha ya ugumu wa mechi hiyo, lakini watapambana kuonyesha ushindani mkubwa wakianzia na ya Ligi Kuu Mei 28 kwenye Uwanja wa KMC Complex kisha na ile ya nusu fainali ya Kombe la FA itakayopigwa Mei 31.

Timu hiyo imepata tiketi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao baada ya Yanga kuifunga JKT Tanzania kwa mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA, hivyo kujihakikishia kumaliza nafasi ya tatu au ya nne msimu huu.

Iko hivi, bingwa wa Kombe la FA anapata tiketi ya kucheza CAF, ingawa kitendo cha Yanga na Simba kujihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika Ligi Kuu kimezipa nafasi Singida na Azam FC kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho.

Ouma aliiongoza timu hiyo Februari 4, 2025 baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miloud Hamdi aliyetambulishwa Desemba 30, 2024 kuondoka kikosini na kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga anayoendelea kuifundisha.

Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa akiwa na leseni A ya UEFA aliondoka Singida bila kuiongoza katika mechi yoyote ambapo alijiunga nayo ili kuchukua nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, 2024.

Tangu Ouma akabidhiwe kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne na pointi 53 amekiongoza katika mechi 11 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo kimeshinda sita, sare mbili na kupoteza tatu huku kikifunga mabao 18 na kuruhusu 10.