Opah Clement ndo basi tena FC Juzrez

Muktasari:
- Opah alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo akitokea Henan Jianye ya China alikocheza msimu mmoja.
KLABU ya FC Juarez ya Mexico imeachana na mshambuliaji wa Kitanzania, Opah Clement baada ya kuhudumu kikosini hapo kwa msimu mmoja.
Opah alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini humo akitokea Henan Jianye ya China alikocheza msimu mmoja.
Kupitia taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa Instagram wa klabu hiyo imetangaza kuachana na nyota huyo wa zamani wa Simba Queens kwa makubaliano ya pande zote mbili.
"Asante sana, Opah tunathamini sana weledi na juhudi zako wakati wa kukaa kwako mpakani," ilisema taarifa hiyo
Kuondoka kwa Opah klabuni hapo kunafanya timu hiyo ibaki na wachezaji wawili wa Kitanzania yaani beki Julietha Singano na mshambuliaji Enekia Kasonga 'Lunyamila'.
Singano aliitumikia Juarez kwa misimu mitatu lakini Lunyamila alitambulishwa kikosini hapo wiki chache zilizopita akitokea Mazaltan ya nchini humo ambako alicheza kwa msimu mmoja tu.
Opah alicheza mechi sita kati ya 17 zilizocheza timu hiyo bila ya kufunga bao wala asisti.
Msimu uliopita akiwa na Jianye ya China alifunga mabao matano na kumaliza msimu akiwa 10 bora za wafungaji mbele ya Yuan Cong aliyeongoza akiwa na tisa.
Ukiachana na Simba Queens 2021/22 alikopata mafanikio makubwa ya soka la wanawake, nyota huyo alichezea Kayseri Kadın ya Uturuki kwa mkopo 2022, msimu uliofuata akasajiliwa Beşiktaş ya nchi hiyo na 2023/24 akiichezea Henan Jianye ya China kwa msimu mmoja.
Kwa ujumla hadi sasa Opah amefunga mabao 16 kwenye timu tatu alizopita tangu aondoke Simba, Jianye na Kayseri Kadin akifunga mabao matano huku Besiktas ya Uturuki akiweka kambani mabao sita.