Kisa Karia, Manara ahojiwa Polisi, aachiwa

Muktasari:
- Manara ambaye ni mwanachama wa Yanga, inaelezwa ametoa maelezo kwa maandishi katika Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam kisha kupewa dhamana.
OFISA Habari wa zamani wa Simba na Yanga, Haji Manara ameshtakiwa polisi na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Leo Ijumaa, Manara aliitwa na Jeshi la Polisi Tanzania kisha kuhojiwa kwa tuhuma za kumdhalilisha Karia mtandaoni.
Manara ambaye ni mwanachama wa Yanga, inaelezwa ametoa maelezo kwa maandishi katika Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es Salaam kisha kupewa dhamana.
Manara alithibitisha taarifa hizo akisema: "Ni kweli nimeshtakiwa, lakini nisingependa kusema chochote zaidi, bado nipo kwenye vikao na mawakili wangu juu ya hili."
Hii ni mara pili kwa Manara kuingia matatani na bosi huyo wa Shirikisho la Soka Tanzania ambapo awali alishtakiwa na kufungiwa na Kamati ya Maadili ya TFF kwa miaka miwili baada ya wawili hao kudaiwa kuzozana kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), kati ya Coastal Union na Yanga uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, mwaka 2022.