Nyota watano wafumua kikosi Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibaden akiwaongoza msimbazi katika mazoezi
Muktasari:
Kocha Mkuu wa Simba inayojiandaa kuikabili Mtibwa Sugar Jumamosi ijayo, Abdallah Kibadeni alisema ujio wa wachezaji watatu wapya kiungo mahiri Henry Joseph, straika Tambwe Amisi na beki Gilbert Kaze kumebadili mambo katika kikosi chake.
BENCHI la Ufundi la Simba limetamka kwamba wachezaji watano wazoefu akiwamo Henry Joseph wana nafasi kubwa kwenye kikosi cha kwanza huku likitaja ‘masuper sub’ watatu wakali.
Kocha Mkuu wa Simba inayojiandaa kuikabili Mtibwa Sugar Jumamosi ijayo, Abdallah Kibadeni alisema ujio wa wachezaji watatu wapya kiungo mahiri Henry Joseph, straika Tambwe Amisi na beki Gilbert Kaze kumebadili mambo katika kikosi chake.
Alisema kuhusu watakaojumuishwa kikosi chake cha kwanza: “Wachezaji wanne wa kigeni tuliowasajili (kutoka Uganda na Burundi ), pia wapo wachezaji walioko Taifa Stars na wengine ambao wataonyesha juhudi.”
Wachezaji wa Simba wa kigeni ni raia wawili wa Uganda, Abel Dhaira na Joseph Owino, Warundi Tambwe Amisi na Gilbert Kaze. Wakati walioko Taifa Stars kwa sasa ni Amri Kiemba, Haruni Chanongo, Jonas Mkude na Henry Joseph.
Kibadeni alikwenda mbali zaidi kwa kutaja ‘masuper sub’ wapya wa Simba: “Nina wachezaji wengi waliosajiliwa, hivyo benchi la super sub litaongozwa na Miraj Adam, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Said Ndemla, William Lucian na Sino Agustino.”
“Ili timu icheze vizuri lazima kuwe na kombinesheni nzuri kwa kuwa kwa kawaida lazima wachezaji wote wacheze pamoja kutafuta matokeo, naamini Tambwe na Kaze wanahitaji muda, tulimsajili Shindika (Henry Joseph) kutokana na ubora wake, ana uzoefu wa kutosha, uwezo wa kukaba, upigaji pasi na nguvu za kupambana akiwa uwanjani,” alisema Kibadeni.
Hata hivyo, kwa hali halisi ilivyo ni kwamba wachezaji kama Andrew Ntalla, Ramadhani Singano ‘Messi’, Hassan Khatib, Rahim Juma, Haruna Shamte (nahodha msaidizi), Abdallah Seseme, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, Ibrahim Twaha ‘Messi’, Marcel Kaheza, Edward Christopher, Zahoro Pazi, Omary Salum, Emil Mgeta, Abou Hashim, Hassan Isihaka na Adeyoun Saleh wanahitaji kufanya kazi kubwa kulishawishi benchi la ufundi ili kuingia katika kikosi cha kwanza mara kwa mara.