Nyota wa zamani wa Spurs, West Ham kusaka vipaji Bongo

Muktasari:
- Kanoute aliyewahi pia kutamba na Sevilla ya Hispania, Lyon ya Ufaransa na timu ya taifa ya Mali, akishinda tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika 2007 akiwaka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa nje ya bara la Afrika kushinda tuzo hiyo ataongoza jopo la kusaka vuipaji katioka michuano hiyo ya vijana.
MSHAMBULIAJI na nyota wa zamani wa klabu za West Ham United na Tottenham Hotspur za England, Frederic Kanoute anatarajiwa kutua nchini ili kusaidia kutafuta vipaji kupitia mashindano ya soka kwa vijana Afrika Mashariki ambayo yatafanyika jijini Arusha.
Kanoute aliyewahi pia kutamba na Sevilla ya Hispania, Lyon ya Ufaransa na timu ya taifa ya Mali akishinda tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika 2007 akiwa mchezaji wa kwanza aliyezaliwa nje ya Afrika kushinda, ataongoza jopo la kusaka vipaji katika michuano hiyo ya vijana.
Ujio wake katika mashindano hayo yanayojulikana kama Chipkizi Cup ambayo yanafanyika kwa mwaka wa 15, ni kumbukumbu nzuri ya kutoa nyota wengi akiwemo beki wa Goztepe ya Uturuki na Taifa Stars, Novatus Dismas yanalenga kuibua chipukizi wenye vipaji.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Desemba 9 hadi 15, mwaka huu yakishirikisha zaidi ya timu 320 kutoka nchi za Afrika Mashariki na nje, ambapo kwa mara ya kwanza timu za soka za Kafue Celtic inayoshiriki Ligi Kuu Zambia na Plateau United inayoshiriki Ligi Kuu Nigeria zitashiriki.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Future Stars Academy (FSA), Alfred Itaeli wanaoandaa mashindano hayo ameiambia Mwanaspoti kwamba Kanouté atakuwa ni miongoni mwa mawakala ambao watakuja kuangalia vipaji vya soka na michezo mingine ambapo atawasili nchini Desemba 11.
Amesema ujio wake ni fursa kwa soka la Tanzania na Afrika Mashariki kwani wachezaji ambao atawachagua watapata nafasi ya kutimiza ndoto za kucheza soka la kulipwa Ulaya, ambapo miaka ya baadaye watakuja kuwa matunda mazuri kwa timu zao za taifa.
"Kwetu ni furaha kuona tunazidi kuwa daraja kwa vijana kutimiza malengo na ndoto zao. Kikubwa tu wachezaji wote ambao watashiriki mashindano haya wapambane ili kupata nafasi ya kuchaguliwa," amesema Itaeli.
Jumla ya wachezaji 4800 wa timu za vijana kuanzia umri wa chini ya miaka tisa hadi 20 wanaume na wanawake watashiriki katika michuano hiyo ambayo itafanyika katika viwanja vya UWC, Agha Khan, St Constantine, TGT na Braeburn, huku ikishirikisha soka, kuogela na kikapu lengo likiwa ni kuibua na kukuza vipaji pamoja na kutangaza utalii wa Tanzania kupitia michezo.