Novatus aipeleka Stars mapumziko kifua mbele

BAO la Frikiki ya moja kwa moja lililofungwa na kiungo Novatus Dismas dakika ya tisa limetosha kuipeleka mapumziko timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikiongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika mechi hiyo ya kirafiki ya Kimataifa inayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novatus alifunga bao hilo baada ya kuangushwa kwa kiungo Feisal Salum ‘Feitoto’ nje kidogo ya boksi la 18 la Afrika ya kati.
Licha ya Stars kutangulia kwa bao hilo lakini mechi ilionekana kuwa ba uwiano sawa wa umiliki wa mpira hususani katikati ya Uwanja.
Novatus, Mbwana Samatta, Nickson Kibabage, Feisal Salum na Kelvin John ni miongoni mwa mastaa wa Stars walioonesha kiwango bora ndani ya dakika 45 za kwanza.
Kipa wa Stars, Metacha Mnata dakika ya 33 alifanya makosa ambayo almanusura Afrika ya kati ipate bao lakini mabeki waliondosha mpira ule.
Hata hivyo mashabiki wachache waliopo uwanjani hapa walionekana kutoridhishwa na kiwango alichokionesha mshambuliaji wa Stars Abdillahie Yusuff kwani muda mwingi alipoteza mipira na kucheza madhambi.
Hadi dakika 45 za mchezo huo zinamalizika, Taifa Stars 1-0 Jamhuri ya Afrika ya kati.