Beki wa Simba awindwa Mashujaa

Muktasari:
- Kazi aliyejiunga na timu hiyo Julai 20, 2023 akitokea Geita Gold, ameshindwa kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue, hivyo kuanza kutafuta changamoto mpya.
UONGOZI wa maafande wa Mashujaa uko katika harakati za kukisuka kikosi kwa ajili ya msimu ujao, ambapo tayari mabosi wa timu hiyo wameanza harakati za kumuwinda beki wa kati wa Simba, Hussein Kazi anayemaliza mkataba wake.
Kazi aliyejiunga na timu hiyo Julai 20, 2023 akitokea Geita Gold, ameshindwa kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue, hivyo kuanza kutafuta changamoto mpya.
Pendekezo la beki huyo wa kati ni la Kocha Mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga anayetaka kuongezewa nguvu eneo hilo baada ya nyota wa kikosi hicho, Ibrahim Ame kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara ya misuli, hivyo kupiga hesabu hizo mapema.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema ni mapema kuzungumzia sasa suala zima la usajili hadi watakapomaliza mechi zilizosalia za Ligi Kuu Bara, ingawa ni kweli kuna maeneo watakayofanyia maboresho.
“Kuna mapendekezo ya benchi la ufundi yaliyowasilishwa na sisi pia kama viongozi tumeanza kufanyia kazi mapema. Hatuwezi kuweka wazi ni wachezaji gani ambao tunawahitaji kwa sasa kwa sababu za kiushindani zilizopo,” alisema Meja Abdul Tika.
Licha ya uzoefu wa Kazi aliyezichezea timu mbalimbali ikiwamo Forester ya Shelisheli kabla ya kurejea na kujiunga na Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania na Geita Gold ameshindwa kupenya mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, mkataba wake Simba unafikia tamati mwisho wa msimu huu ambapo hadi sasa hakuna mazungumzo mapya ya kuongeza mwingine.