Prime
Dili la Camara mikononi mwa Diarra

Muktasari:
- Lakini, nyuma ya hilo makipa hao pia wana mengi, ingawa kwa Camara huenda akawa na jipya ambalo kwa wengi hapa nchini litawaacha vinywa wazi wakishangaa kwani sio la kawaida.
KUNA lile bato la Djigui Diara, kipa mwenye rekodi zake bora katika Ligi Kuu Bara kwa misimu minne na yule wa Simba, Moussa Camara aliyetua Msimbazi msimu huu ambao wanawania ubabe wa 'cleen sheet' mwisho wa msimu.
Lakini, nyuma ya hilo makipa hao pia wana mengi, ingawa kwa Camara huenda akawa na jipya ambalo kwa wengi hapa nchini litawaacha vinywa wazi wakishangaa kwani sio la kawaida.
Iko hivi, Camara ana kibarua cha kupambana mechi tatu zilizobaki asiruhusu bao ili ajihakikishie kubeba tuzo mbili kwa mpigo huku mtu aliyeshikilia hilo akiwa ni Diarra.
Simba ina mechi tatu zilizobaki kwenye ligi msimu huu ambazo ni dhidi ya KenGold (Juni 18, 2025), Kagera Sugar (Juni 22, 2025) na Yanga (Juni 25, 2025) ambapo Camara akifanikiwa kucheza mbili pekee bila ya kuruhusu bao, basi atakuwa kinara wa klinshiti kwani hivi sasa anazo 17, akimuacha Diarra mwenye 15.
Kwa sasa, Camara hapa nchini anavizia tuzo ya kipa bora, pia huko kwao Guinea amewabananisha makipa wanne tofauti akiwania nyingine.
Camara yupo kwenye orodha ya makipa watano watakaowania tuzo ya kipa bora wa Guinea msimu huu zinazoandaliwa na waandishi wa habari zikijulikana kama Tuzo za CIS Media.
Katika tuzo hizo, Camara anachuana na Mory Keita anayeichezea Hafia ya Guinea, Mohammed Camara (Asante Kotoko ya Ghana), Sekou Sylla (Horoya ya Guinea) na Yello Dialo (Renaisance ya Chad).
Kwenye tuzo hizo, mpinzani mkubwa wa Camara ni Sylla ambaye aliyeiongoza Horoya kukaribia kuchukua ubingwa.
Sylla akiwa na Horoya msimu huu amekusanya cleen sheets 15 ndani ya michezo 22.
Camara amewahi kuchukua tuzo hiyo akiwa na Horoya alipofikisha cleen sheets 19 na hadi sasa anazo 17 akiwa na Simba, hivyo bado mbili kuifikia rekodi hiyo.
Faida nyingine inayombeba Camara ni kutokana na kipa huyo kuwa chaguo la kwanza kuanzia klabuni kwake na timu ya taifa, vitu ambavyo kwa mujibu wa wachambuzi wa michezo nchini humo wanampa nafasi kubwa kubeba tuzo hiyo.
Hapa nchini pia Camara anavizia tuzo kama hiyo akiendelea kukimbizana na Djigui Diara wa Yanga ambaye yuko chini yake akiwa na klinshiti 15.
Tangu ametua Simba kipa huyo amefanikiwa kufanya mageuzi makubwa akipindua ufalme wa Aishi Manula aliyekuwa chaguo la kwanza kwa muda mrefu na msimu huu, Camara amecheza mechi 25 kwa dakika 2250 akiruhusu mabao 11.