Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya ubingwa Bara… Simba, Yanga zakabana koo

KOO Pict
KOO Pict

Muktasari:

  • Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, iliitanguliza Simba kuweka mabao matatu dhidi ya KenGold dakika ya 20, 22 na 26, kisha yenyewe ikalipa kwa kuweka mbili dakika ya 31 na 35 dhidi ya Tanzania Prisons. Matokeo ya mwisho Tanzania Prisons 0-5 Yanga na KenGold 0-5 Simba.

MWENDO wa weka niweke ulikuwa katika mechi za raundi ya 29 za Ligi Kuu Bara zilizochezwa Jumatano hii ambapo kulikuwa na vita kubwa ya kujitengenezea mazingira mazuri ya kubeba ubingwa na kuepuka kucheza mechi za mtoano (play offs) ya kutoshuka daraja. Hiyo ni baada ya KenGold na Kagera Sugar kushuka daraja moja kwa moja na kuacha nyingine zikipambana kubaki salama.

Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, iliitanguliza Simba kuweka mabao matatu dhidi ya KenGold dakika ya 20, 22 na 26, kisha yenyewe ikalipa kwa kuweka mbili dakika ya 31 na 35 dhidi ya Tanzania Prisons. Matokeo ya mwisho Tanzania Prisons 0-5 Yanga na KenGold 0-5 Simba.

Kabla ya hapo, wakati Simba ikiwa mbele kwa mabao 3-0 dhidi ya KenGold, ilikaa kileleni kwa muda wa takribani dakika 11 kabla ya Mudathir Yahya kuifungia Yanga bao katika dakika ya 31 na kuirejesha timu hiyo sehemu yake ya kwanza.

Wakati mechi zote nane za raundi ya 29 zikitarajiwa kuanza, Yanga ilikuwa kileleni na pointi 73, ikifuatiwa na Simba iliyokusanya pointi 72, hivyo kuongoza kwa mabao 3-0 dhidi ya KenGold, ikawaweka Wekundu kileleni kwa pointi 75, ghafla wakajikuta wameshushwa pale Yanga ilipopiga bao la kwanza na kufikisha pointi 76.

Mabao ya Simba katika mchezo dhidi ya KenGold uliochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, yalifungwa na Kibu Denis (dk 20 na 26), Elie Mpanzu (dk 22), Leonel Ateba (dk 36) na Jean Charles Ahoua (dk 75).

Kwa upande wa Yanga iliyocheza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, mabao yalifungwa na Mudathir Yahya (dk 31), Clatous Chama (dk 35), Pacome Zouzoua (dk 56 na 76) na Israel Mwenda (dk 61).


5-0 ZATAWALA

Wakati Simba na Yanga mechi zao zikivuna mabao mengi kwa kila moja kushinda 5-0, ushindi huo pia ulipatikana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam pale Azam FC ilipoichakaza Tabora United  kwa kipigo kama hicho.

Mabao ya Azam yalifungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ katika dakika ya 11, Gibril Sillah (dk 17 na 30), Idd Seleman ‘Nado’ (dk 45+1) na Nassor Saadun (dk 89). Azam sasa imejihakikishia nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 60 ambazo haziwezi kufikiwa na Singida Black Stars yenye 56 ikibaki mechi moja.


DODOMA JIJI 1-2 SINGIDA BS

Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji walipoteza kwa mabao 1-2 dhidi Singida Black Stars ambapo wageni walifunga kupitia Arthur Bada dakika ya kwanza na Jonathan Sowah (dk 6) kwa penalti. Bao la Dodoma Jiji lilifungwa na Idd Kipagwile dakika ya 41 kwa penalti. Licha ya kupoteza, Dodoma Jiji imebaki salama, haitacheza play off, huku Singida Black Stars ikibaki nafasi ya nne.

Bao la Sowah liliendeleza rekodi yake ya kibabe tangu aliposajiliwa katika dirisha dogo ambapo sasa amefunga mabao 12 katika mechi 13 za Ligi Kuu Bara akiwa na Singida Black Stars. 


COASTAL UNION 1-0 FOUNTAIN GATE

Bao la Lucas Kikoti la dakika ya 60 akiliweka kimiani kwa penalti, lilitosha kuipa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Fountain Gate, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Ushindi huo umeifanya Coastal kuwa salama na kuepuka presha ya kuangukia play off.


MASHUJAA 1-1 KMC

Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, bao la dakika ya 90 lililofungwa na mshambuliaji wa KMC, Akram Mhina, lilikuwa na maana kubwa kwa timu hiyo ambayo imejihakikishia kubaki kwenye ligi baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Mashujaa ambayo ilianza kufunga katika dakika ya 11 kupitia kwa Mundhir Vuai.


PAMBA JIJI 1-0 JKT TANZANIA

Zabona Mayombya bao alilofunga katika dakika ya 40, limefufua matumaini ya Pamba Jiji kusalia kwenye ligi ikifikisha pointi 33 baada ya kuichapa JKT Tanzania 1-0 kwenye Dimba la CCM Kirumba, Mwanza.


NAMUNGO 0-0 KAGERA SUGAR

Mchezo pekee ambao haukuwa na bao ni huu uliochezwa lwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo mkoani Lindi ambapo suluhu hiyo imewafanya wenyeji kuendelea kubaki kwenye presha ya play off wakati Kagera Sugar ikiwa tayari imeshuka daraja.