Njooni muone mabao

UTAMU wa Ligi Kuu Bara unarejea upya leo baada ya kusimama kwa muda kupisha mechi za Kombe la Shirikisho (ASFC), wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba watakapokuwa wenyeji wa JKT Tanzania, huku timu zote zikiwa moto katika kutupia nyavuni.

Timu hizo zitavaana katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Simba inakutana na maafande hao waliowang’oa mabingwa wa zamani wa Tanzania, Mtibwa Sugar kwenye ASFC, ikitoka kupata ushindi mtamu dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia kuifumua African Lyon kwenye mechi yao ya Kombe la Shirikisho na kutinga 16 Bora.

Mechi hiyo ya marudiano kwa timu hizo itapigwa kuanza saa 1:00 usiku, huku Simba ikisaka alama nyingine tatu ili kuweza kuwasogelea vinara, Yanga waliopo kileleni na alama zao 49, pointi saba zaidi ya walizonazo wao Wekundu wenye michezo mitatu mkononi kwa sasa.

Hesabu za ubingwa na maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh wiki hii ni mambo mawili yanayoilazimisha Simba kushinda mechi hiyo ya leo.

Ushindi kwa Simba ni muhimu katika mbio za ubingwa kwani utawafanya wapunguze pengo la pointi baina yake na Yanga wanaoongoza kubakia nne huku wakiwa na faida ya kubakiwa na mechi mbili za viporo.

Hilo limethibitishwa na kocha wa Simba, Didier Gomes aliyesema wanahitaji ushindi dhidi ya JKT Tanzania ili wajiweke pazuri kwenye mbio za ubingwa.

“Tuna michezo mitatu sasa, akili yetu ni kuendelea kufanya vizuri ili tuweze kutetea ubingwa wetu tunatakiwa kushinda ili tuongoze Ligi hili ndio muhimu zaidi kwetu,” alisema Gomez.

Sio tu kwenye suala la ubingwa, ushindi pia utasaidia kuwaweka Simba kwenye hali nzuri kisaikolojia katika maandalizi yao ya mchezo wa raundi ya tatu ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh utakaochezwa huko Khartoum Sudan, Machi 5.

Kwa JKT nao, ushindi ndio kitu kikubwa na cha muhimu kwani utawafanya wafikishe pointi 27 na kusogea hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi wakati sasa wapo katika nafasi ya 10 ambayo sio salama kwao kwani wapo juu ya mstari wa hatari kwa pointi tatu tu.

Historia inaonyesha kuwa Simba wamekuwa wakitamba pindi wakutanapo na maafande hao katika mechi za ligi ikitoka na ushindi kuliko wenzao, kwani hata kwenye mechi yao ya kwanza iliyopigwa mjini Dodoma, Mnyama alitakata kwa kuinyoa JKT kwa mabao 4-0.

Katika mechi tano za mwisho walizokutana, Simba imeibuka na ushindi mara nne, ikifunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili wakati JKT imeshinda mechi moja tu.

Hata hivyo, historia hiyo isiyovutia dhidi ya Simba haionekani kuwapa wasiwasi JKT ambao wamesema hawataipa nafasi katika mchezo wa leo.

“Yaliyotokea nyuma yamepita na sasa hii ni mechi nyingine na ukiangalia kila timu ina mabadiliko hivyo wachezaji na benchi la ufundi akili yetu tumeielekeza katika mechi hii.

“Tunatambua kwamba tunakutana na timu nzuri lakini huu ni mchezo. Timu ambayo itakuwa imejiandaa vizuri itapata ushindi na naamini uwezo wa kushinda dhidi ya Simba tunao,” alisema Kocha wa JKT, Mohamed Abdallah ‘Bares’.

JKT inawategemea Rashid Mandawa, Mwinyi Kazimoto, Michael Aidan na Danny Lyanga na wengine walioing’oa Mtibwa kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 2-2 ndfani ya dakika 90 kuitetemesha Simba iliyoifumua Lyon mabao 3-0 na zote kuingia 16 Bora itakayochezwa kati ya Aprili 3 na 4 ili kusaka timu nane za kutinga robo fainali.