Lamine, Sarpong kumbe balaa

LICHA ya Deus Kaseke kuwa kinara wa mabao wa Yanga akifunga sita, lakini nahodha wake, Lamine Moro na Michael Sarpong wamefunika kati ya nyota wa kigeni wanaokipiga Jangwani kwa kutupia nyavuni, huku Meddie Kagere wa Simba akiendeleza moto kwa msimu wa tatu mfululizo.

Lamine na Sarpong raia wa Ghana ni kati ya wachezaji 10 wa Yanga waliosajiliwa msimu huu, huku kila mmoja amefunga mabao manne, wakiwaongoza wageni wenzao akiwamo Kipa Faruk Shikhalo na straika Fiston Abdulrazack ambaye bado hajagusa nyavu hadi sasa.

Waghana hao wanaongoza wenzao sita waliochangia mabao 24 kati ya 34 ya Yanga msimu huu akiwamo Yacouba Songne raia wa Burkina Faso mwenye manne pia, Wakongo Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda wenye matatu kila mmoja sawa na Carlinhos kutoka Angola, kisha Mrundi Saido Ntibazonkiza kitupia mawili na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima akifunga moja hadi sasa.

Kwa upande wa Simba, Kagere ameendelea kutisha akiwa kinara akifunga tisa, akiwaongoza wageni wenzake saba waliochangia jumla ya mabao 26 kati ya 42 ya timu yao, akifuatiwa na Mzambia, Clatous Chama aliyefunga sita, Mkongoman Chriss Mugalu (4) na Mghana Bernard Morrison (3).

Wageni wengine wenye mabao ni Luis Miquissone kutoka Msumbiji aliyefunga mawili, huku mabeki Mkenya Joash Onyango na Pascal Wawa wa Ivory Coast wakifunga bao moja moja, huku Mzimbabwe Perfect Chikwende, Mganda Taddeo Lwanga na Mzambia Larry Bwalya wakiwa ndio pekee wasio na mabao Msimbazi katika Ligi Kuu mpaka sasa, huku John Bocco akiwaongoza wazawa kwa kufunga mabao nane kati ya 16 waliochangia ndani ya Simba, huku upande wa Jangwani Kaseke ameongoza wazawa kuchangia mabao 10.