Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nguvu ya soka hulinda afya bora za watoto

Muktasari:

Moja ya athari za hali hii nchini hapa ni watoto kuwa na unene unaopindukia ambao hatima yake huwaathiri moja kwa moja hadi wanapokuwa watu wazima na kushindwa kupungua.

MABADILIKO ya mfumo wa maisha duniani yana faida kadhaa,  lakini inaelekea kuna hasara zake pia.

Ulimwengu wa sayansi na teknolojia umekuja na mengi kiuchumi, kijamii na pia katika mfumo mzima wa utamaduni.

Kama kuna kitu ambacho viongozi wa kisiasa na wa michezo pia wanahofia athari zake sasa na kwa kizazi kijacho ni watoto kutulia majumbani.

Kwa hapa London na Uingereza kwa jumla, imekuwa kawaida kwa watoto kukaa ndani muda mwingi, sababu moja ikiwa baridi ya nje, lakini nyingine ikiwa ni kuzoea michezo ya kwenye kompyuta au wanayounganisha kwenye TV,  PlayStations.

Watoto wakishatoka shule huishia kwenye michezo hiyo isiyohusisha mazoezi ya mwili na ikiwa hawaendi shule huanza ‘shughuli’ hiyo asubuhi wakikatisha nyakati za kujisafisha na kula.

Moja ya athari za hali hii nchini hapa ni watoto kuwa na unene unaopindukia ambao hatima yake huwaathiri moja kwa moja hadi wanapokuwa watu wazima na kushindwa kupungua.

La pili, ambalo linawaumiza viongozi wa soka ni kwamba vipaji au fursa za kuwaendeleza watoto hao kisoka hupotea.

Pengine wenzetu hawa wanaanza kupata majawabu juu ya kipi kinachowatatiza katika soka au kwa nini hali ya England inakuwa dhaifu ikilinganishwa na mataifa kama Hispania, Ujerumani, Italia na wengine waliowekeza kwenye soka la watoto na vijana.

Ilivyo ni kwamba, mtoto akishawasha hiyo michezo  kwenye televisheni au kompyuta ni vigumu kuondoka hapo na kama wazazi au walezi hawapo huweza hata kusahau kula.

Nimeshuhudia watoto wanaoshindwa hata kuamua iwapo waende haja pale wanapobanwa kwa kupenda michezo hiyo kupita kiasi. Kitu kinachoathiri akili namna hiyo ni hatari kubwa!

  Kwa kuwa soka ina nguvu na inakua, pengine itaweza kutumiwa kubadili mfumo huu mpya wa maisha, ambao usipodhibitiwa utawaambukiza hata watoto wetu Tanzania, kama haijaanza kutokea.

Njia ya kuzuia hili ni kuwahamasisha watoto na vijana kutotazama soka majumbani mwao, kushiriki kwenye klabu za michezo shuleni na wikiendi na pia wazazi kuwachukua walau mara mbili kwa mwezi kwenda kushuhudia timu za mijini kwao au hata za mbali zaidi.

Nasema hivyo kwa sababu naona ongezeko kubwa la watoto wanene na wavivu wasioweza hata kutembea vyema siku hizi.

Nimepata pia bahati ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa michezo hapa nchini kuhusu hali hiyo na wanaonyesha wasiwasi mkubwa ikiwa hali hii haitadhibitiwa.

Inasikitisha kuona watoto hao wakiendelea kulishwa vyakula vya kuwanenepa halafu wanakaa tu darasani kusoma wakitoka wanakaa kucheza kwa kubofya na kuzungusha vitufe mikononi mwao tu.

Matokeo yake ni kufutuka miili na kuharibika macho, ambapo idadi kubwa ya watoto pia sasa imeanza kuvaa miwani kwani wanaumizwa na mwanga mkali wa kwenye televisheni na kompyuta wanakokaa kwa muda mrefu, wengine wakizisogelea karibu sana.

Soka imekuwa ikitoa mwangwi wa hali ya maisha katika jamii, ambapo sasa England wanalia kwamba wana wachezaji wachache wanaotamba kwenye Ligi Kuu ambao wamezaliwa na kukuzwa hapa Uingereza.

Uhamasishaji bila shaka una nafasi yake na pia jinsi makocha, mameneja na wakurugenzi wa soka wanavyoweza kuwa wabunifu kuwateka watoto kutoka michezo hiyo na kuwaingiza kwenye soka.

Ukocha ni kipaji na pia lazima kocha awe mhamasiahaji na karisma na mvuto wa kubadili mawazo ya watu na kuwaingiza kwenye hali tofauti.

Sunderland walipomfukuza Martin O’Neil kama kocha wao mwaka jana, walisema, pamoja na sababu nyingine kwamba uwanjani ni kama vile hakuwapo.

O’Neil alikuwa akisimama tu kwenye eneo lake akiona timu inafungwa, hana cha kuwaita wachezaji wake wala kuwapanga upya kwa kubadili mfumo.

Kwa jumla, lazima tuseme kwamba hapa England lazima viwango vya soka viboreshwe maana hata kupata kocha Mwingereza kwa timu ya taifa haikuwa kazi ndogo. Wengi wanaonekana hawana sifa. Angalia timu za Ligi Kuu England, makocha wengi ni wa kigeni na wa hapa timu zao hazifanyi vizuri sana.

 Hata hivyo, tunatakiwa kuzama na kuangalia ngazi za chini ya soka si Ligi Kuu tu. Huko nako bado hakuna jitihada toshelezi kwa sababu ukusanyaji vijana, ung’amuaji vipaji na uendelezaji umekuwa si wa kuridhisha.

Licha ya hivyo makocha katika ngazi hizo pia ni wachache na pengine wanakosa kile kinachotakiwa, japokuwa ni kweli Chama cha Soka (FA) England na Bodi ya Ligi Kuu wamekuwa wakisemwa kujaribu kuongeza ushiriki.

Takwimu za karibuni zaidi za FA zinaonesha ongezeko dogo tu la asilimia 0.83 mwaka jana katika idadi ya timu za vijana zinazofungamanishwa nao kote nchini.

Bodi ya Ligi Kuu inasema kwamba katika msimu uliopita kulikuwa na ongezeko la asilimia 26 la mauzo ya tiketi kwa watoto na vijana ambapo zilifikia 58,546.

Wanafikiri kwamba kuongezeka kwa watoto na vijana wanaokwenda uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu, ni chanzo, kama nilivyosema awali, cha watoto na vijana kushawishika kuanza kucheza.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha vinginevyo, kwamba wanaongezeka wanaokwenda mpirani kutazama mechi za Ligi Kuu lakini hawaongezeki huko kwenye kucheza kwenyewe.

Mema yaliyoachwa na Michezo ya Olimpiki ya London katika upenzi wa michezo ni kitu kimoja lakini kila msimu wa Ligi Kuu hutoa burudani ya kipekee inayotakiwa kushawishi watoto na vijana kujitumbukiza kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, tusisahau pia kwamba baada ya mamilioni ya wadhamini kutumbukizwa kwenye Ligi Kuu England, vituo vya televisheni vinaonyesha mechi nyingi zaidi moja kwa moja.

Athari yake ni ipi? Vijana na watoto ‘wavivu’ hufutilia mbali mpango wa kwenda uwanjani kujionea badala yake hujimwaga kwenye sofa (wengine wakilala kabisa, si kusinzia) kutazama soka kama wanavyokaa kwenye PlayStation.

Wanafanya hivyo ili kuepuka kutoka nje, kutembea, kupanda magari binafsi, mabasi au treni na kufika kukaa majukwaani, kuwapa moyo wale wa timu zao, kuruka ruka au kushangilia kama wengine.

Huamua kubaki ndani, ambako hewa ni ile ile ya kuwasha ‘heater’ tangu asubuhi hadi usiku (kama si msimu wa kiangazi) ili wawe kwenye Play Station hadi mpira ukianza wahamie huko na ukimalizika warudi kwenye PlayStation au kuangalia katuni kabisa.

Hii ni tofauti kabisa na miongozo ya kiafya na wadau wa soka kwamba wazazi na walezi wanatakiwa kuwashawishi watoto kutoka nje mara kwa mara hata baada ya shule au wikiendi ili kupata hewa nzuri, hata kama kuna baridi si kuna sweta? Pia kuna vituo vingi vya michezo ya ndani lakini takwimu za mahudhurio si nzuri.

Kadiri ya asilimia 30 ya watoto wa Uingereza wana uzito uliopitiliza au wenyewe wanavyosema ‘obesity.’

Utafiti wa Idara ya Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo unaonyesha kwamba idadi ya watoto kati ya umri wa miaka mitano hadi 10 wanaoshiriki michezo imeshuka kwa asilimia 10 tangu mwaka 2009/2010.

Inadaiwa pia kwamba takriban asilimia 85 ya wasichana  na asilimia 73 ya wavulana wenye umri wa miaka 13 hawafanyi mazoezi ya saa moja yanayoshauriwa na wataalamu wa afya.

Japokuwa lawama zote haziwezi kwenda kwa FA, wafadhili na wadhamini wanaotumbukiza fedha nyingi kuinua soka kuanzia ngazi za chini, kama vile McDonald’s, Carlsberg, Budweiser na Mars wanasikitika jinsi fedha zao zinavyopotea huku afya ya watoto wa taifa ikianguka, wazazi na walezi wakidhani unene uliopindukia ni afya.

Ni wazi kwamba sasa wakati umefika kwa wadau wa soka, afya na siasa kuungana kuona nini cha kufanya. Nilimaliza majuzi tu mada yangu juu ya uhusiano wa siasa na soka na kipi kinachoweza kufanywa. Hivyo hili ni jukwaa maridhawa la kutazamwa kwa ajili ya manufaa makubwa, kwani limekuwa sasa ni suala mtambuka.

Bila afya nzuri hakuna soka nzuri wala mafanikio ya timu za taifa za vijana na wakubwa, hakuna ufanisi katika kazi.

Haitakuwa ajabu miaka 10 ijayo kuona wachezaji wa England wamezidi kupungua kwenye Ligi Kuu yao, wasije wakageuka tena na kusema Waafrika wanavamia huku na kuwanyima fursa watu wao. Waafrika wanajua wana vipaji lakini pia wanahitaji fedha, hivyo hutumia fursa zozote zinazotokea kwa nguvu zote kupata mafanikio na kuzikomboa familia zao kwenye umaskini.

Waingereza wanapoangalia jinsi ya kufuzu kwenda Brazil na kurejesha heshima ya taifa hili kimichezo, lazima watumie mbinu mbalimbali kuzuia uvivu unaowafunika.