Ndo hivyo, Sancho kulazimisha dili la Man United

MANCHESTER, ENGLAND. SOMA hiyo. Jadon Sancho anaamini atakuwa mchezaji wa Manchester United kabla ya dirisha kufungwa Jumatatu.

Winga huyo Mwingereza, Sancho mwenye umri wa miaka 20, amewataka washauri wake wa mambo ya uhamisho “kuondoa vikwazo vyote” ili kukamilisha dili lake la kutua Old Trafford akitokea Borussia Dortmund.

Sancho hakujumuishwa kwenye kikosi cha Dortmund katika mchezo wa Kombe la Ujerumani dhidi ya Bayern Munich juzi Jumatano.

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer anazidi kupata uhakika wa kunasa huduma ya mchezaji huyo chaguo lake kwenye dirisha hili kabla halijafungwa.

Ripoti za kutoka Ujerumani, Dortmund wameshakubali kumpoteza supastaa wao huyo, licha ya kudai hadharani kwamba wanaamini atabaki.

Kuna mtu wa karibu kabisa na Sancho, alisema: “Anataka dili hili kukamilika.

“Amemwambia wakala wake na washauri wake kufanya kila wanaloweza kuhakikisha jambo hilo linakamilika.

“Wanapambana kwa ajili yake aondoke.”

Dortmund imeripotiwa kwamba inataka walau Pauni 80 milioni kwanza na kisha nyongeza nyingine.

Chanzo cha karibu kabisa za kuhusu mchakato wa dili hilo la uhamisho lililochukua muda mrefu kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, kinafichua kwamba Sancho atawagha-rimu Man United Pauni 95 milioni, tofauti na kiwango cha Pauni 108 milioni ambacho Dortmund inataka kulipwa.

Wasimamizi wa mambo hayo ya uhamisho wamekuwa kwenye mazungumzo ya kukamilisha dili hiyo kimyakimya ili kuhakikisha linakamilika kabla ya dirisha kufungwa Jumatatu ijayo.

Chanzo hicho kilifichua: “Kuna jambo dogo sana linachelewesha...ni suala la nani aanza kwanza.

“Man United itaongeza ofa yao au Dortmund itakubali ofa ya pesa ya chini? Manchester United wao inafikiria kupeleka ofa ya mwisho kabisa kwa ajili ya mchezaji huyo hadi kufikia jana Jumatano na inaamini itavuka vikwazo vyote na kufanya mambo kukamilika haraka.”

Kuwasili kwa Sancho huko Old Trafford kutafungua milango ya winga, Daniel James kwenda kujiunga na Leeds United na jambo hilo linaweza kuwa kwa mkopo wa msimu mzima au dili la jumla kama wababe hao wanaonolewa na Marcelo Bielsa watakuwa na mkwanja wa kunasa huduma yake jumla.