Ndemla, Ajibu someni ujumbe wenu Kibadeni amewapa makavu

STRAIKA wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Abdallah King Kibadeni ameweka wazi kwamba wachezaji wengi wa sasa hawajitambui na anatamani angalau enzi zao zingekuwa sasa.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Kibadeni anaweka wazi kwamba wachezaji hao wanalipwa fedha nyingi na wana chaneli nyingi za kufanya makubwa na kujiendelea, lakini hawajielewi na wanahitaji msaada mkubwa kama hawajapotea zaidi.
“Zamani mpira ulikuwa ni sehemu ya kukusanyika, kukutana na watu kufurahi kutatua matatizo na kusaidiana na kushindana pia, lakini pia wakati huo tulikuwa hatulipwi, hela yote ilikuwa inakwenda kwa klabu, lakini sasa hivi mpira unalipa sana duniani,” anasema huku akizungumzia enzi zao hakukuwa na wachezaji wa kigeni.
“Sasa wanataka kuleta soko la ushindani, lakini halinufaishi wazawa kwa sababu unachukua mchezaji wa kigeni unalipa fedha nyingi za kigeni kuliko mchezaji wa nyumbani, hili pia linatusumbua sana Watanzania
“Mimi sipingi ujio wao, lakini unaweza kuleta wachezaji 10 au 9 ama 7 unataka nini? Kwa mfano, walimu kwenye mashule wapo lakini wanakimbilia kuchukua walimu kutoka nje mfano Kenya ama Uganda kwa sababu wanaongea sana kiingereza, hawa walimu wazawa utawapeleka wapi?
“Kinachotakiwa kufanya ni kutumia wataalamu wa kutosha wazalishe walimu wengi waende kusoma,’’ anasema Kibadeni, ambaye astashahada yake ya ukocha aliisomea kule Ujerumani na mafunzo mengine alipata Brazil.
“Tatizo nchi yetu ni kubwa na walimu ni wachache, nakiri kwamba walimu wazuri wapo ila tupo wachache sana,” anaongeza mchezaji huyo wa zamani wa Simba, ambaye hat trick yake kwenye mechi ya watani haijawahi kuvunjwa mpaka sasa.
ALIWAUWA YANGA
Anasema mechi dhidi ya Yanga ambayo Simba alishinda 6-0 mwaka 1977 na yeye akifunga mabao hat trick katika mchezo huo, hawezi kuisahau.
“Hii haiwezi kufutika katika historia ya maisha yangu ya mpira, kwani hiyo rekodi mpaka hivi sasa, hakuna mchezaji ameifuta. Zinapokutana timu hizo mbili kongwe hapa nchini, na mimi nakumbuka nilifanya kazi, na sio mimi tu, lakini kama timu tulikuwa tumejipanga twende tukawaadhibu wale mabwana.”
MECHI AKIWA STARS
“Nakumbuka tulikwenda kucheza Ghana, tulitoa sare ya mabao 2-2, tulianza kuwafunga wao kisha wakarudisha na kutufunga bao la pili, lakini dakika za mwishoni za mchezo tulisawazisha, na mfungaji wa goli hilo nikiwa ni mimi”
Mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Sudan. “Tulijikuta tumevaa jezi za kijani na njano, Sudan nao wakaja na rangi hiyo hiyo, sasa ikawa mpira unachelewa kuanza, Rais (Mwalimu, J. K Nyerere) alikuwepo uwanjani na muda ukawa unakwenda, ikabidi waamuzi watuambie sisi wenyeji tuvue fulana, na kweli tulivua na kubaki matumbo wazi.
“Kwa hiyo, tukajipanga matumbo wazi, watu walishangaa kwa kweli, basi Rais akawa anashuka kutoka jukwaani, akawa anakimbia watu walimshangilia sana. Hii ni wakati wa kuja kutupa mikono, tulicheza kidogo ila baada ya muda jezi zikafika tukavaa,”.
AKIWA KOCHA
Wakati akiwa kocha wa Simba, anakumbuka walicheza mechi moja na Yanga pale Uwanja wa Taifa, Simba akapoteza mashabiki wakakimbilia nyumbani kwa baba yake Ilala, walipofika wakapiga mawe dukani kwao.
“Walifanya fujo sana ikanibidi siku ya pili nikaamua kujiuzulu kuifundisha Simba tena mbele ya waandishi wa habari, nakumbuka kambi yetu tuliweka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mashabiki wa Simba hawakuja nyumbani kwangu Sinza ila walikwenda kwa mzee wangu pale Ilala.”
TIMU NDOGO, KUBWA
“Raha ya kuzifundisha timu kubwa ni kwamba, zina uwezo wa kifedha na miundombinu mizuri kwa kazi yako kama mwalimu inakuwa nyepesi. Wana uwezo pia wa kuiweka timu kambini na wachezaji wanakuwa kitu kimoja.
Timu nyingine wanangoja siku moja ama mbili ndio wanaweka kambi, kwa hiyo changamoto inakuja hapo, uwezo wa kazi yako kama mwalimu ndipo unaonekana, timu kubwa wanaweza kukupa mipira 40 ama 30, ukija kwa timu ndogo wanakupa mipira minne ama mitano tu.”
AMZUNGUMZIA FRANK KASANGA
Anasema mchezaji huyo alikuwa na uwezo na akili za ajabu, na pia alikuwa akifuata kile ambacho kocha anamtaka kukifanya kwa wakati huo, hivyo akiwa kocha wake alikuwa akipenda kumtumia iwe Simba au Taifa Stars.
“Huyo alikuwa mchezaji wangu tangu enzi za Red Star, alikuwa mahiri sana na fundi haswa, achana tu na kuwa na pumzi lakini, anaweza akawa sehemu ya hatari na yeye akautaka mpira licha ya kwamba anaweza akanyang’anywa. Pia, alikuwa anaweza kucheza nafasi ya ulinzi na akapanda kwenda kusaidia mashambulizi. Hivyo, nilikuwa naye Simba na pia katika timu ya Taifa kwa kiwango chake,” anasema Kibaden.
KIKOSI CHAKE BORA WAKATI ANACHEZA
Wakati anacheza Simba, kikosi hakikuwa kinabadilika sana, golini alikuwa anacheza Mambosasa na Omary Mahadhi, ukiondoa wengine ambao wametangulia kucheza kabla yao. Mechi zote ngumu na zenye mikikimikiki mingi alikuwa akipewa Mahadhi na Mambosasa.
“Beki namba mbili alikuwa anacheza Daudi Salum, ama Shabani Baraza, beki namba tatu alikuwepo Marehemu Mohamed Kajori na Hamis Askari. Kwa hiyo tunatazama na ugumu wa mechi, namba nne kulikuwa na Alo Mwitu pale katikati, Mohamed Bakari ‘Tall’ akisaidiana na Chogo, wote walikuwa wakali.
“Namba sita alikuwa Khalid Abedi, alikuwa hana mpinzani, wakati mwingine alikuwa anacheza Aluu Ally, namba saba alikuwepo William Mwaijibe, yaani bila hao watu maana yake Simba haipo, namba nane alicheza Haidary Abeid ama Ismail Mwarabu, lakini Abeid alikuwa anaongoza kwanza.
Namba tisa alikuwepo Adamu Sabu na Jumanne Masnichi, hao ndio kwa kawaida wanaanza. Tunatazama aina ya mechi na ugumu wake kwa mfano, mechi ya ufundi anacheza Jumanne na mechi ya nguvu anacheza Adam.
“Namba 10 nilikuwa mimi, wakati mwingine alikuwepo Kesi Manangu (Marehemu), lakini Manangu alikuwa akicheza tu iwapo naumwa ama nikiamua mwenyewe kuwa aanze kucheza, na mwingine alikuwa Abdalah Mwinyimkuu, namba 11 alikuwepo Abasi Dilunga akisaidiana na marehemu Omary Gumbo.
“Hicho ndicho kikosi cha wakati huo ambapo hapakuwa na mgeni hata mmoja, pia ni watu waliokuwa wanajulikana hata kifamilia, maana hata ukifanya vurugu ama lolote baya basi walezi ama wazazi wako watafahamu, habari zitafika nyumbani.
“Kwa hiyo tulikuwa tunaogopa kufanya vitu vingine vya ajabu ili usivunje heshima ya wazee na watu wanajua kuwa huyu ni mtoto wa nani, hivyo wanakwenda kutoa taarifa,”
KUHUSU NDEMLA
“Kusema ukweli Ndemla ni mchezaji mzuri, ila mwenyewe hajui anajionaje. Ndemla ukimpa nafasi, anaweza kufanya vizuri kuliko mtu mwingine unayemtumia kutoka nje. Lingine ni kwamba, hawa wachezaji wetu hawajitambui, huwa hawafuati taratibu ama kuupa heshima mpira kwa kuwa ndio unaowatambulisha mtaani na kuwafanya kuthaminika na kupendwa.
“Sasa unakuta mchezaji ana nidhamu mbovu na walimu wetu hawa wa kigeni sio sawa na wazawa hawajui kama Ndemla au mchezaji fulani anatoka Buguruni, yeye anataka mtu amfanyie kazi,” anasema.
Anasema tatizo jingine ni kwa wachezaji wenyewe kutojitambua, kwa mfano Ibrahim Ajib anajua sana mpira ila hafuati taratibu za mpira, anafanya mpaka kocha ashindwe kumpa nafasi. Mwalimu anampenda mchezaji kwa jinsi anavyojitolea, hawezi kumchukia mchezaji bila sababu.
“Mchezaji ni lazima ujitume ili kujisaidia wewe mwenyewe ili mwalimu akuone unafaa, lakini hawa walimu wageni hawawaamini wachezaji wazawa ndio maana wanafuata wachezaji wa nje.
“Lakini, mimi ninapenda zaidi wachezaji wazawa kwa kuwa unaweza kumueleza kwamba, umekosea hili ama lile. Kwa mfano mchezaji amezoea kuchelewa kurudi nyumbani, kwa hiyo unatakiwa kuwa na nidhamu hata nje ya uwanja ufanye jambo lipendeze kwa jamii.”
KIKOSI BORA WAKATI ANAFUNDISHA SIMBA
Magolikipa ni Mohamed Mwameja na Omary Mahadhi, mabeki ni Baraza, Gaga, George Masatu, mbele walikuwa wakina Niko Kiondo, Niko Njohole, pia walikuwepo wakina Roho mtu, George Lukas, Zamoyoni Mogela, Malota Soma.
AKADEMI
“Nina akademi yangu inaitwa KIFA-Kibadeni Football International Academy. Ila kwa sasa tumefunga kwasababu ya janga hili la corona, walikuwa wanakuja vijana kuanzia miaka nane hadi kumi ila pia wanakuja hata wakubwa.
Lengo la kuanzisha Academi hiyo iliyoko Chamazi, Dar es Salaam, ni kuwaibua akina Kibadeni wengine ambao watakuja kuwa mastaa wapya kwenye Ligi Kuu Bara, Taifa Stars na ligi zingine za madaraja ya chini. Vijana wengi wana vipaji hivyo, tunavindeleza.ji lisaidia Taifa.”