Mbeya City yavamia dili la beki Simba

Muktasari:
- Kazi aliyejiunga na timu hiyo Julai 20, 2023, akitokea Geita Gold, ameshindwa kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya mabeki wenzake, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue, hivyo kuanza kutafuta changamoto sehemu mpya.
MABOSI wa Mbeya City wameanza kuingilia kati dili la beki wa kati wa Simba, Hussein Kazi ambaye mkataba wake na kikosi hicho cha Msimbazi umefikia tamati msimu huu, baada ya awali nyota huyo kuanza mazungumzo ya kujiunga na Mashujaa FC.
Kazi aliyejiunga na timu hiyo Julai 20, 2023, akitokea Geita Gold, ameshindwa kupenya katika kikosi cha kwanza mbele ya mabeki wenzake, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue, hivyo kuanza kutafuta changamoto sehemu mpya.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza viongozi wa Mbeya City wameanza mazungumzo ya kina na kambi ya mchezaji huyo kwa ajili ya kuipata saini yake kwa msimu ujao, hivyo kuanzisha vita upya na Mashujaa ambayo imeonyesha pia nia.
Akizungumza na Mwanaspoti Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma alisema mipango ya kukisuka kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao imeanza, japo ni mapema sana kuweka wazi ni mchezaji gani wanayemuhitaji katika dirisha hili kubwa.
“Kipindi hiki ni cha kuviziana kwa sababu leo nikikuambia tunafanya mazungumzo na mchezaji fulani ambaye pia washindani wetu wanamuhitaji, maana yake tunakaribisha vita zaidi, hivyo acha tufanye mambo yetu kwa umakini mkubwa,” alisema Ally.
Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu Kazi huenda dili lake la kwenda Mashujaa likakwama, baada ya mabosi wa kikosi hicho kuinasa saini ya aliyekuwa beki wa kati wa Kagera Sugar, Mohamed Mussa Salum ‘Jecha’ ili kuichezea timu hiyo msimu ujao.
Licha ya uzoefu wa Kazi aliyezichezea timu mbalimbali zikiwemo za Forester FC ya Shelisheli, kabla ya kurejea nchini na kujiunga na Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania na Geita Gold, ila ameshindwa kupenya mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
Mbeya Ciy imemaliza Ligi ya Championship ikiwa nafasi ya pili na pointi 68, baada ya kushinda mechi 20, sare nane na kupoteza mbili, nyuma ya Mtibwa Sugar iliyoibuka bingwa mpya msimu huu, kufuatia kuibuka kidedea na pointi zake 71.
Mbeya City inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa FC, ameirejesha tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2022-23, ikianza mawindo ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao ili kuongeza ushindani.