Nasser, Prince mguu sawa mbio za magari Uganda

Muktasari:
- Ikija na bango la Shell V Power, raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari Afrika inajulikana kama Pearl of Africa Rally na inatua Uganda baada ya kutamatika kwa ufunguzi Kenya, Machi mwaka huu.
MTANZANIA Yassin Nasser ataondoka wa pili katika mashindano ya raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari Afrika, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na waandaaji zikiwa zimebaki siku nane kabla ya kuanza Mei 10.
Ikija na bango la Shell V Power, raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari Afrika inajulikana kama Pearl of Africa Rally na inatua Uganda baada ya kutamatika kwa ufunguzi Kenya, Machi mwaka huu.
Nasser na Prince Charles Nyerere ndio Watanzania pekee katika mashindano hayo ambayo yatachezwa katika nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nssser ambaye gari yake imepewa namba 40 ubavuni ataongozwa na msoma ramani Mganda Ally Katumba ndani ya gari aina ya Ford Fiesta.
Akijnadi kwa jina la Moil Team, Nasser anaongoza kwa pointi kuelekea raundi ya pili ya ubingwa wa Afrika.
Mtanzania mwingine, Prince Charles Nyerere ataondoka wa 10 na gari aina ya Mitsubish Evolution X ambayo pia itakuwa na namba 10 ubavuni.
Prince Nyerere ataongozwa msoma ramani kutoka Rwanda, Faustin Rutabingwa.
Watanzania hao ni miongoni mwa washiriki 52 waliothibitisha ushiriki hadi Jumatatu, wiki hii.
Wa kwanza kuondoka, kwa mujibu wa orodha ya uanzaji ni Mkenya Karan Patel ambaye ataongozwa na msoma ramani Tauseef Khan wakiendesha gari aina ya Skoda Fabia.
Licha ya kushindwa kumaliza katika raundi ya ufunguzi nchini Kenya, Patel anaondoka wa kwanza kama bingwa mtetezi kwa sababu ndiye alikuwa mshindi wa jumla wa raundi zote 2024
Nyuma ya Mtanzania Nasser, atakayeondoka namba 3 atakuwa ni Mkenya Saman Singh Vohra ambaye ataongozwa na msoma ramani Drew Sturrock.