Namungo yashtuka, haifanyi tena kosa

UONGOZI wa Namungo umesema wapo makini katika maandalizi ya mechi zao za makundi hasa za ugenini wakihofia isije kuwakuta kile walichokutana nacho nchini Angola walipokwenda kwa ajili ya mchezo dhidi ya Primiero de Agosto.
Namungo ilikumbana na sintofahamu nchini humo kwa kuzuiwa uwanja wa ndege kwa madai ya nyota wao watatu - Lucas Kikosi, Khamis Faki na Fred Tangalu kuwa na corona pamoja na mtendaji wao mkuu, Omar Kaya ambao waliwekwa karantini siku zaidi ya 10.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaya alisema kwa sasa wamejua namna gani ya kujilinda katika hatua inayofuata kutokana na kadhia waliyokumbana nayo na kujikuta wakipata wakati mgumu nchini humo.
“Ishu ya karantini kwanza tulipelekwa kwa madai ya kuwa na corona, lakini hata kuonyeshwa karatasi yetu ya vipimo hii hakuna, sasa hata sisi kujua tulikuwa nayo au la ni ngumu ila tunamshukuru Mungu tumerudi wazima,” alisema Kaya.
Alisema kutokana na changamoto hiyo na ugeni waliokuwa nao wamepata somo linalowafanya wajilinde zaidi. “Kundi letu ni gumu, wapinzani wetu wote wana uzoefu zaidi ya sisi lakini mpira sasa ni dakika 90 ndani ya uwanja,” alisema na kusisitiza kuwa kwa kukitambua hilo watahakikisha wanacheza kwa tahadhari kubwa ili kupata matokeo nyumbani na ugenini.
“Michuano hii inatangaza nchi na pia wachezaji wanapata nafasi ya kuonekana na kujiuza zaidi katika timu kubwa.” Kuhusu bajeti ya sasa katika hatua hiyo, Kaya alisema hawana bajeti maalumu kutokana na sintofahamu ya nchi nyingine juu ya corona, hivyo wanatumia gharama kubwa.
“Lakini ndio tunapambana kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” alisema.
Kuingia makundi kumeifanya Namungo kujihakikishia kuzoa dola 275,000 (zaidi ya Sh600 milioni).