Nabi aushtukia mtego Simba...Apiga mkwara nyota wake

SIMBA imetua Dar es Salaam ikitoka Bukoba, huku mashabiki wa Yanga wakichekelea wakiamini biashara imeisha, lakini Kocha Nasreddine Nabi amewapiga marufuku mastaa wake kushangilia akisema matokeo ya Simba na timu nyingine katika Ligi Kuu Bara wala hayawahusu.
Kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia, amewapiga ‘stop’ mastaa wake baada ya kikao kizito alichofanya nao kabla ya kwenda jijini Mwanza kwa mchezo wao wa 32 Bora wa Kombe la ASFC dhidi ya Mbao unaopigwa kesho.
Nabi aliliambia Mwanaspoti anafahamu kwa sasa wamewaacha Simba kwa tofauti ya pointi 10 baada ya mechi 13 za Ligi Kuu Bara, lakini akawazuia wachezaji wake kufuatilia matokeo ya wapinzani wao na badala yake wazingatie mambo yao.
“Nimewaambia wachezaji sitaki kusikia hata wanazungumza ishu za Simba kwani matokeo yao hayatuhusu na nimewataka wazingitie na kufikiria zaidi mechi zetu zinazotukabili,” alisema Nabi na kuongeza;
“Nimewaambia kabisa nikimkuta mchezaji yeyote anafanya hivyo au mtu yeyote katika benchi langu la ufundi akiijadili Simba au timu nyingine juu ya matokeo yao nitawapa adhabu zilizopo kwenye miongozo yao ya kazi.”
“Yanga tuna mechi zetu ambazo sasa zitazidi kuwa ngumu, nimewaambia kuanzia sasa kila mchezo utakaokuwa mbele yetu utakuwa ni sawa na fainali ngumu ambazo ni lazima tuzishinde,” alisisitiza Nabi aliyeiongoza Yanga katika mechi 20 za Ligi bila kupoteza tangu Yanga ilipofungwa bao 1-0 msimu uliopita na Azam katika mechi iliyopigwa Aprili 25, mwaka jana.
Yanga kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 35 baada ya mechi 13, ikiwa ni tofauti ya pointi 10 kwani Simba katika mechi kama hizo imekusanya pointi 25, lakini Nabi alisema bado hawatakiwi kuidharau Simba kwani makosa yoyote watakayofanya katika kudondosha pointi yanaweza kuwapa presha.
Alisema msimamo aliowapa wachezaji wake unatakiwa pia kufanyika kwa mashabiki wa timu hiyo na hata uongozi kwani kazi bado haijaisha katika kutimiza malengo yao.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa naye amepigilia msumari akisema wao kama viongozi hakuna kurudi nyuma huku akijivunia ubora wa sasa wa kikosi chao.
“Nafikiri kwa watu wanaojua mpira huwezi kuendelea kushangilia anguko la wanaoshindana na wewe.”