Nabi atoa angalizo kambini

Muktasari:

  • Kiufundi, Nabi alisema tayari wachezaji wake wanajua nini watafanya uwanjani kulingana na mchezo husika kwani tayari kawapa mbinu za kuhakikisha dakika 90 zikimalizika wanatoka kifua mbele na si kwa unyonge.

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akitoa angalizo kambini kabla ya pambano hilo litakalopigwa Jumapili hii.

Kocha Nabi aliliambia Mwanaspoti kwamba mbali na kutaka utulivu kwa vijana wake, lakini kubwa alichopania ni kuhakikisha raha nyumbani kabla ya kwenda kurudiana nao akihitaji ushindi wa mabao yasiyopungua matatu.

Alifafanua jinsi ambavyo fainali hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) inavyozungumziwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na hamu ya mashabiki kuona timu yao inawapa raha, hilo ndilo linamsukuma kutengeneza mbinu ya nyumbani kwanza.

Jambo la kwanza anataka kuondoa presha kwa wachezaji kujua hata kama mashabiki wakijaa uwanjani lengo lao ni kuhitaji ushindi na mchezo hautakuwa mrahisi, kwani kwa hatua waliofikia mataifa mengine yanawaogopa, hivyo wanahitaji kujipanga zaidi.

"Mashabiki wanaohamasishana wakijaa uwanjani kiu yao ni moja tu, kuona Yanga inawapa raha kwa kushinda, sasa mimi sitaki liwe bao moja yawe angalau matatu, hata kule tukikwama huku tayari tumewapa kicheko," alisema Nabi na kuongeza;

"Fainali hiyo ni kubwa utatazamwa na mataifa mengi, ndio maana najaribu kuwaandaa wachezaji ili wacheze kwa kiwango kikubwa ambacho kitaipa heshima klabu kuingia kwenye historia ya aina yake."

Kiufundi, Nabi alisema tayari wachezaji wake wanajua nini watafanya uwanjani kulingana na mchezo husika kwani tayari kawapa mbinu za kuhakikisha dakika 90 zikimalizika wanatoka kifua mbele na si kwa unyonge.

"Mbali na ninachowapa wachezaji wenyewe wanatambua umuhimu wa mchezo huo, wanahamasishana wenyewe kwa wenyewe imefikia hatua wananipa hamasa hadi mimi, lengo ni kulinda blandi ya Yanga," alisema.

Yanga itavaana na USM Alger Jumapili katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni baada ya kupenya kwa kuing'oa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla la mabao 4-1 na kurudiana nao Juni 3 jijini Algers.