Nabi asuka hesabu kali kwa Waarabu

Muktasari:

  • Nabi amesisitiza tangu atue Tanzania hajawahi kuwa mtu wa kukata tamaa na anajipanga kubadilisha mambo katika kikosi chake kwenye mchezo wa marudiano ugenini baada ya kulala nyumbani kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya USM Algier lakini Kuna akili akaifanya kwa wachezaji wake.

MASHABIKI wa Yanga wamegawanyika, wapo ambao wamekata tamaa wakiona ni kama timu yao imeshakosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na wako wengine wanaona timu yao itarudisha furaha yao kwenye mchezo wa ugenini na hawa ndio wako pamoja na kocha wao, Nasreddine Nabi.

Nabi amesisitiza tangu atue Tanzania hajawahi kuwa mtu wa kukata tamaa na anajipanga kubadilisha mambo katika kikosi chake kwenye mchezo wa marudiano ugenini baada ya kulala nyumbani kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya USM Algier lakini Kuna akili akaifanya kwa wachezaji wake.

Raia huyo wa Tunisia ameliambia Mwanaspoti anafahamu Yanga ina kiu kubwa ya kutaka taji la Afrika lakini msimu huu mpaka sasa hana anachowadai wachezaji wake na wamefanya kazi kubwa.

Hata hivyo, kocha huyo amewataka wachezaji kufanya mambo mawili tu makubwa kwenda kurudia maajabu yao kwa kucheza kwa jihadi ugenini kujaribu kupindua meza mbele ya USM Alger kisha warudi kuchukua taji la Azam Shirikisho (ASFC).

"Najivunia sana wachezaji wangu, inawezekana tukifanya makosa katika mchezo wa hapa nyumbani (dhidi ya USM Alger) lakini haipotezi shukrani zangu kwa kikosi hiki, wamefanya kazi kubwa msimu huu," alisema Nabi.

"Tukifika mazoezini Leo (jana jioni) nitawaambia kwamba hawapaswi kuvunjika moyo wainua vichwa juu wajivunie hatua ambayo wameipiga msimu huu, lakini wanatakiwa kwenda kucheza kiume Algeria.

"Hili sio mara ya kwanza kwao kufanya makubwa walifanya tukiwa Tunisia, Bamako, Lubumbashi, Nigeria na Rostenburg sehemu zote hizi wengi waliona kama Yanga haitatoka salama watu walidhani hatutofanya vizuri lakini tukawashangaza.

"Huwa napenda morali ya wachezaji wangu wanapocheza ugenini, bado mechi haijaisha tutakwenda tena kuipigania Yanga, bado kuna picha kubwa ya mashabiki wetu waliofurika uwanjani hapa nyumbani wakitoka kuumizwa na matokeo, wale ndio tunaokwenda kuwapigania kujaribu kurudisha furaha yao.

"Wako ambao wamepoteza uhai na kuumia ili waje kutupa nguvu tuna kitu tunatakiwa kuwafariji na kuwapa pole wale ambao wamepoteza ndugu yao, tuko hapa kwa ajili ya mashabiki na klabu hii, walituamini lakini bado tuna nafasi ya kwenda kubadilisha mambo," alisema Nabi.

Aidha Nabi aliongeza anajua ni aina gani ya mabadiliko atayafanya kwenye kikosi chake kukabiliana na mbinu za wapinzani wao kwenye mchezo huo utakaopigwa Juni 3, jijini Algers.

Wakati kikosi hicho kikianza maandalizi hayo ya mchezo wa marudiano tayari upande wa utawala wameshamtanguliza mtu mmoja mzito kwenda kuandaa mazingira ya timu yao nchini Algeria.

Mwanaspoti linafahamu hadi muda huu unaposoma habari hii Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji, tayari yupo nchini humo akipambana kuandaa mazingira ya timu yao kabla ya kikosi hicho kuanza safari Alhamisi Juni Mosi kwa Ndege ya Shirika la Tanzania kutafuta ushindi wa kuanzia mabao 2-0 na kuendelea.