Nabi aanza na Saido, Mukoko akitumia dakika 37, msosi wa Shikhalo wamshtua

KOCHA mpya wa Yanga, Nesreddine Nabi aliishuhudia timu hiyo juzi usiku ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Gwambina kwenye Uwanja wa Mkapa, lakini akasema kwamba; “nimefurahi.”

Baada ya pale, akakaa kikao cha dakika kumi na viongozi mbalimbali palepale uwanjani kisha akajichanganya vyumbani kwenda kujuana na vijana wake.

Awali, kabla ya kuanza kwa mchezo huo alitambulishwa kidogo kwa wachezaji kisha wakaingia uwanjani. Baadaye sasa ndio akakaa nao dakika 37 muda huo wao wakiendelea kufuturu kwa vile wale waliofunga muda uliwakuta uwanjani.

Jamaa aliingia kwanza akachonga na kocha aliyemkuta, Juma Mwambusi wakabadilishana mawazo kwa dakika saba.

Akawasalimia wasaidizi wake katika benchi lake akionyesha furaha kujiunga nao akiambatana na msaidizi wake mpya, Sghir Hammadi ambaye alitua naye juzi mchana.

Baada ya hapo akakutana na wachezaji wawili wa kigeni, kiungo Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda akifurahi kusikia wametokea DR Congo ambako alifanya kazi kisha wakaongea kwa dakika kama nane kwa lugha ya Kifaransa.


ATUA KWA YACOUBA

Nabi alitua kwa Yacouba Sogne ambapo hapo pia Kifaransa kiliendelea kwa dakika kadhaa akijaribu kumuelezea alichokiona huku pia akimsikiliza mshambuliaji huyo.

Akasogea kwa kiungo Carlos Carlinhos huku shida ikawa wote Kiingereza chao kilikuwa cha kubahatisha zaidi na hakukaa sana. Huku wachezaji wakiendelea kufuturu akamsogelea kipa Farouk Shikhalo akamwambia “Farouk hiki chakula kingi sana sitachukua changu njoo hapa tuongee.” Kisha wakateta kwa dakika kadhaa huku akimpongeza kwa kuwa na mchezo mzuri.

Alikutana pia na wachezaji wazawa wakiwemo Kibwana Shomari na Dickson Job huku akitaka kujua aliumia nini katika mchezo huo ambapo pia alikutana na nahodha msaidizi, Bakari Mwamnyeto na hata Deus Kaseke.

Kikao cha mwisho cha kocha huyo alikitumia kwa dakika 20 akikaa pamoja na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akiongea naye mambo mengi huku kila mmoja akionekana kumwongelesha mwenzake wakibadilishana mawazo.


MSIKIE MWENYEWE

Baada ya vikao hivyo, Nabi aliliambia Mwanaspoti kuwa amefurahi kuiona timu hiyo kwa macho yake.

“Kwanza nimpongeze kocha niliyemkuta, amefanya kazi kubwa hapa, unapoona timu inashinda hivi lazima utoe pongezi kwa kocha na hata wachezaji, ni watu wanaopambana kwa timu yao,” alisema Nabi ambaye ana uzoefu na soka la Afrika.

Kocha huyo raia wa Tunisia alisema amegundua kwamba wachezaji wako sawa kwa stamina, lakini shida ipo katika ufundi ambao lazima kuna kazi ya kufanya.

“Stamina na pumzi naona iko sawa, nimefurahi, lakini yapo maeneo ambayo tunatakiwa kuyaboresha zaidi ili iwe timu ambayo itatupa tunachotaka,” akasema.

“Hapa kwenye ufundi ndio sehemu ambayo tunatakiwa kuanza napo, kuna mambo hayapo sawa, nafikiri kwa sasa ni kuelekea moja kwa moja kwenye kazi kwa ujumla, kuna wachezaji ambao nawaona wana ubora lakini wapo ambao tunatakiwa kuwaongezea kitu.”

Juzi baada ya mechi hiyo, Nabi alikubali kuwapa mapumziko ya usiku huo wachezaji wa timu hiyo wakapumzike majumbani kwao, lakini akawapa habari kwamba jana mchana kila mmoja alitakiwa kambini na jioni hiyohiyo kazi inaanza.