Mzungu Serengeti Boys ayeyuka, Mrundi atajwa

Muktasari:
Mkurugenzi wa Ufundi (TFF), Ammy Ninje, alipotafutwa ili kuthibitisha taarifa za Mrundi huyo na kukwama kwa mzungu, alisema hawezi kutolea ufafanuzi kwa sasa kwani ni mapema.
ULE mpango wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kutaka kuongeza kocha mzungu kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana U-17, Serengeti Boys umeyeyuka na sasa anatajwa Mrundi.
TFF ilitangaza kuwa na nia ya kuliongezea nguvu benchi la timu hiyo itakayokuwa mwenyeji wa Fainali za Afcon U-17 zitakazofanyika kati ya Aprili 14-28, huku ilielezwa kocha huyo angetoka Uingereza.
Hata hivyo, Mwanaspoti limezinyaka taarifa kocha huyo Muingereza imeshindika kuja nchini na badala yake TFF imeanza kumtupia macho Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije.
Inaelezwa TFF imevutiwa na uwezo wa Mrundi huyo aliyekuwa akitajwa kunyatiwa na Simba ili kwenda kumsaidia Patrick Aussems katika kutengeneza vijana na kuwapa makali uwanjani.
Ndayiragije aliisaidia Mbao iliyopanda Ligi Kuu kufika fainali ya Kombe la FA na akiwa na KMC kwa sasa ameifanya timu hiyo kuwa tishio licha ya ugeni wake katika ligi hiyo wanayoicheza kwa mara ya kwanza.
Mkurugenzi wa Ufundi (TFF), Ammy Ninje, alipotafutwa ili kuthibitisha taarifa za Mrundi huyo na kukwama kwa mzungu, alisema hawezi kutolea ufafanuzi kwa sasa kwani ni mapema.
“Najua watu wa habari mnataka kuwa wa kwanza kuandika mambo haya, ila ukweli bado hatujakaa na kuchanganua majina, muda ukifika tutatangaza na kila mmoja atajua nani atasaidiana na Oscar (Milambo),” alisema Ninje.
Akizungumzia kuhusu kutokuja kwa kocha wa kigeni, alikiri imeshindikana na ndio maana wameamua kutafuta kocha ambaye analijua vizuri soka la Bongo.
“Imeshindika kuja kwa kocha Muingereza na sasa tunaangalia kocha aliyepo katika Ligi Kuu anayewafahamu vizuri wachezaji wa kitanzania, ili aweze kuwaongezea nguvu katika benchi la Serenegeti Boys,” alisema.