Mrembo amponda Januzaj kwa ubahili

Mrembo Melissa McKenzie
Muktasari:
- Mrembo Melissa McKenzie amemponda vibaya kinda huyo kufuatia ahadi yao ya kwanza ya kukutana huku wakitarajiwa kuwa wapenzi, baada ya Januzaj kumpeleka sehemu ya misosi ya bei rahisi.
WAKATI jina la kinda wa Manchester United, Adnan Januzaj likiendelea kuchomoza kwa kasi ndani ya uwanja, tayari nje ya uwanja staa huyo mzaliwa wa Ubelgiji ameanza mbwembwe zake, lakini huku akianza vibaya.
Mrembo Melissa McKenzie amemponda vibaya kinda huyo kufuatia ahadi yao ya kwanza ya kukutana huku wakitarajiwa kuwa wapenzi, baada ya Januzaj kumpeleka sehemu ya misosi ya bei rahisi.
Januzaj alimpeleka Melissa katika mgahawa wa Nando’s ambao chakula chake ni cha gharama ya chini na mwishowe aliishia kumnunulia demu huyo chips kuku, vyote vikiwa na gharama ya Pauni 18 tu (Sh45,000 za Tanzania).
Kama vile haitoshi, Melissa alikerwa vilivyo na kitendo cha Januzaj kushindwa hata kulipia sehemu ya maegesho ya magari huku akimuacha yeye akilipa licha ya kuwa mpenzi wake huyo mtarajiwa ni staa anayelipwa kiasi cha Pauni 30,000 (Sh75 milioni) kwa wiki.
Melissa pia alishangazwa na kitendo cha Januzaj kutokea katika mihadi hiyo akiwa na ‘tracksuit’ pamoja na raba za uwanjani. Yeye alimchukua sehemu Januzaj baada ya kinda huyo kushushwa sehemu ya mihadi na mama yake mzazi.
“Sijawahi kukutana na mtu bahili kama yeye katika maisha yangu. Kwanza nilifurahi sana tulipopeana ahadi ya kukutana kwa mara ya kwanza. Tulikutana katika mitandao ya kijamii na nilivaa vizuri huku nikijipakaa vipodozi vilivyonigharimu Pauni 30,” anasema Melissa.
“Nilitazamia aje kunichukua na gari la kifahari, lakini niliishia kumchukua mimi katika gari langu la kizamani la Fiesta. Mimi ndiye niliyelipa ada ya maegesho. Baadaye alinipeleka Nando’s. Sura yangu ilinishuka,” anasema Melissa.
“Mara nyingi napenda kwenda pale kula na rafiki zangu. Sikutazamiwa kwenda pale nikiwa katika mapenzi na staa wa Manchester United, sana sana kwa jinsi nilivyovaa nguo zangu na viatu virefu.”
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Januzaj alilipa kiasi cha Pauni 18 tu kwa ajili ya chakula hicho cha jioni na baadaye wakaenda kwenye hoteli ya hadhi ya nyota tatu ambapo kwa pamoja walitazama kipindi cha The X Factor.
Melissa anadai kwamba baadaye Januzaj aliomba kurudishwa nyumbani ifikapo saa tatu kamili usiku. Kutokana na hali hiyo, penzi lao halikwenda popote.
Hata hivyo, kufuatia siri hiyo iliyochomolewa na Mellisa, mrembo huyo alipondwa na mashabiki mbalimbali wa soka duniani kwa kile kilichodaiwa kuweka tamaa ya pesa mbele kuliko mapenzi.
Pia Melissa alipondwa vilivyo na mastaa wawili wa timu ya taifa ya England, Andros Townsend wa Tottenham Hotspurs na Raheem Sterling wa Liverpool ambao walishangazwa na tabia za Melissa.
Alikuwa ni Townsend aliyeanza kuponda kwa kuandika katika mtandao wake wa Twitter akisema; “Wanawake wa aina hii wanasababisha nijisikie vibaya. Unapelekaje mambo haya katika gazeti? Sijui.”
Kama vile haitoshi, Townsend alimkejeli Melissa kwa kuandika; “Kwanza Nandos ilikuwa bora sana kwake. Mimi ningemnunulia Freddo (pipi) na kumwambia arudi kwao.”
Aliyefuatia kuponda alikuwa Sterling ambaye aliandika kwa lugha ya kebehi katika mtandao wake wa kijamii akisema: “Ni stori iliyotengenezwa kwa sababu huyu msichana alitaka paja la kuku akaishia kupata (ng’wara) mguu.”
Kama vile haitoshi, Raheem aliyeonekana kukasirishwa zaidi na kauli ya Melissa aliandika tena katika mtandao wake akisema; “Dada kama ulitaka kipande zaidi cha kuku ungeomba tu.”
Wakati Townsend na Sterling wakimtetea Januzaj, Kampuni ya Nando’s imetumia mwanya huo kujitangaza zaidi baada ya kumpa ofa Januzaj ya kula bure akienda na mpenzi mwingine siku nyingine.
Winga wa Crystal Palace, Jason Puncheon alikwenda katika mtandao wake wa Instagram na kuweka kopi ya makala ya Mellisa huku akiandika: “Januzaj amekuwa mwanaume halisi. Amenifurahisha. Ni kitu gani kinachowafanya hawa watu wadhani kwamba inambidi atumie pesa sana kwa sababu anazo nyingi!”
Kiungo wa Norwich City, Bradley Johnson naye aliungana na mastaa wengine wa Ligi Kuu England kumponda Melissa huku akiandika kwa kebehi: “Inaonyesha ni aina gani ya msichana alivyo. Nadhani anastahili kuku wa senti 99 na chips.”
Wakati wenzake wakiponda, mlinzi wa Manchester United, Rio Ferdinand alitumia fursa hiyo kufanya kama mzaha kwa kuweka picha aliyopiga na Januzaj katika mechi moja ya mchezo wa kikapu jijini London huku akiandika kama vile alikuwa anamwelekeza Januzaj njia ya kwenda Nando’s.