Moses Phiri aifuata Yanga Dar

MSAFARA wa timu ya Zanaco wenye watu 30, akiwamo winga matata Moses Phiri wametua Dar tayari kuwapa burudani mashabiki wa Yanga katika kilele cha tamasha la Siku ya Mwananchi, linalofanyika kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Phiri, mmoja ya wachezaji waliokuwa wakiwindwa na Yanga pamoja na wapinzani wao wa jadi, Simba, kabla ya dili zake kubuma, ni kati ya wachezaji 20 wa Zanaco wanaokuja na kikosi hicho kwa ajili ya mchezo wa kuhitimisha tamasha hilo la Yanga kwa kuvaana na wenyeji wao.
Mbali na Phiri, kikosi cha Zanaco kina majembe mengine kama Racha Kola, Mangani Banda, Christon Jere, Tiberius Lombard, Zito Tembo, Kebson Kamanga, Peter Job Banda, Belchance Makiese, Golden Mafwenta, Peter Kalote.
Wengine ni Jimmy Nakena, Kevin Owusu, Nafwa Mwansa, Lassa Gradi Kiala, Kelvin Kapumbu, Ernest Mbwewe, Souleymanou Moussa, Romaric Pitroipa na Damiano Sam Kola, huku benchi lao la ufundi likijumuisha watu saba na viongozi watatu.
Zanaco wanakuja kuipima Yanga itakayotambulisha nyota wake wapya na mchezo huo kuwa kipimo kizuri kwa Kocha Nasreddine Nabi, huku pia pambano hilo likiwa kama la kisasi baina ya timu hizo zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kuwakilisha nchi zao.
Zanaco imeitoa Yanga mara mbili katika michuano ya CAF mwaka 2006 na 2017.