Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morocco afichua mambo matatu akimrudisha Job Stars na kuwaacha Msuva, Samatta

Muktasari:


  • Kwenye makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Karume Ilala, Dar es Salaam, kocha Morocco alitaja majina ya wachezaji 23 kwa ajili ya michezo miwili ya kuwania nafasi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

KAIMU kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' amefichua mambo matatu katika uchaguzi wa kikosi cha timu hiyo alichokitangaza leo, Jumatatu akimrejesha beki wa Yanga, Dickson Job na kuwaacha Simon Msuva na nahodha Mbwana Samatta, ambaye hata hivyo aliwasilisha barua ya kujiuzulu kuitumikia Stars.

Kwenye makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Karume Ilala, Dar es Salaam, kocha Morocco alitaja majina ya wachezaji 23 kwa ajili ya michezo miwili ya kuwania nafasi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.

Morocco anayekaimu nafasi ya Adel Amrouche ambaye alifungiwa kwa tovu wa nidhamu katika fainali zilizopita za Afcon kule Ivory Coast, alisema mambo aliyozingatia katika uteuzi wake ni utimamu wa mwili kwa kila mchezaji, kiwango kwa sasa na vile watakavyoendana na mipango yake kiufundi katika michezo hiyo ambayo ni dhidi ya Ethiopia na Guinea.

Taifa Stars ambayo ipo kundi H, itatupa karata yake ya kwanza kwenye kinyang'anyiro hicho Septemba 4 kwa kuanzia nyumbani dhidi ya Ethiopia kisha kusafiri hadi Guinea siku sita baadaye (Septemba 10) kukabiliana na wenyeji hao.

"Najua kuwa Watanzania wangependa kuona wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa nje wakiitwa lakini lazima wajue kuwa sisi kama walimu kuna mambo ambayo huwa tunazingatia na wachezaji wapo wengi hivyo orodha ingekuwa ndefu.

"Muda ni mchache sana kwa hiyo tumetazama wachezaji ambao wapo tayari moja kwa moja kuja kutumika, ni muhimu kuwa na wachezaji ambao wapo tayari, sisi kama benchi la ufundi kazi yetu itakuwa kuingiza mbinu tu kwa ajili ya kutafuta matokeo katika michezo hiyo," amesema kocha huyo.

Wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi hicho makipa ni; Ally Salim (Simba), Aboutwalib Mshery (Yanga) na Yona Amos (Pamba).

Mabeki ni Nathaniel Chilambo, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo (Azam), Mohammed Hussein 'Tshabalala' (Simba), Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca', Bakari Mwamnyeto, Nickson Kibabage (Yanga), Abdulmalik Zakaria (Mashujaa).

Viungo ni Adolf Mtasingwa (Azam), Himid Mao (Talaal El Geish, Misri)  Novatus Dismas (Goztepe, Uturuki), Mudathir Yahya (Yanga), Hussein Semfuko (Coastal Union), Edwin Balua (Simba) na Feisal Salum 'Fei Toto' (Azam).

Washambuliaji; Wazir Junior (Dodoma Jiji), Clement Mzize (Yanga), Cyprian Kachwele (Vancouver, Canada) na Abel Josiah (TDS TFF Academy).

Wachezaji hao wataingia kambini kuanzia Agosti 28 kwa ajili ya michezo hiyo.


KUHUSU SAMATTA, MSUVA

Akizungumzia kuwaacha Samatta na Msuva ambao wamekuwa wakiongoza safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars, kocha Morocco amesema alifanya nao mazungumzo kabla ya uchaguzi wa kikosi hicho hivyo hakuna shida yoyote.

"Samatta ni nahodha wetu, kuna masuala anayashughulikia hata Msuva pia kama wangekuwa tayari kwa michezo hiyo basi nisingesita kuwajumuisha kikosini lakini pia muda ni mchache sana," amesema.

Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kuwa Samatta kwa sasa anapambana kupata maskani mapya baada ya kocha wa PAOK, Razvan Lucescu kuonyesha hana mipango naye kwa ajili ya msimu huu. Samatta pia aliwahi kuwasilisha barua ya kujiuzulu kuichezea Taifa Stars, barua ambayo hata hivyo, imepingwa na TFF ambayo ilisema itazungumza naye na kwamba nahodha wa taifa hawezi kuachwa astaafu kienyeji.

POAK imeliondoa jina la nahodha huyo wa Taifa Stars kwenye orodha yao ya wachezaji katika mfumo wa wachezaji ambao watatumika katika ligi na kwa upande wake Simon Msuva ameendelea na program zake binafsi huku akisubiri muda wa kujiunga na timu yake mpya ya huko Iraq, Al Talaba SC.


JOB FRESHI

Licha ya kipindi fulani beki wa Yanga, Dickson Job kufungiwa vioo na maneno kuwa mengi ikiwemo kuhisiwa kuwa pengine kuna tatizo kati yake na kocha Morocco, kaimu huyo amesema huu ni wakati wake na amaanini kwa kushirikiana na wachezaji wengine atakuwa na mchango kwenye kikosi hicho.

"Job ni mchezaji mzuri na naamini atakuwa msaada, hayo mengine ni maneno tu ya mtandaoni," amesema kocha huyo.