Mnamjua Bocco vizuri lakini

JOHN Raphael Bocco, nani asiyemfahamu. Amezaliwa miaka 29 iliyopita, kwa sasa ni mmoja wa mastaa wakubwa katika mchezo wa soka. Alianza kucheza soka miaka 11 iliyopita akianza na timu ya Kijitonyama FC na mwaka 2007 aliichezea Cosmo kabla ya baadaye msimu huo huo katika Ligi Daraja la Kwanza alijiunga Azam FC na kuisaidia kuipandisha Ligi Kuu 2007-2008.
Mwanaspoti linakuletea mambo ambayo hukuwa unayafahamu kuhusu nyota huyu.
KLABU NNE TU
Kama hujui tu, Bocco amecheza timu nne tu hadi sasa ikiwamo Kijitonyama FC, Cosmopolitan, Azam FC na sasa Simba akiwa kama nahodha wake akiendeleza makali yake.
Alianza na Kijitonyama FC kwa mafanikio kisha akatua Cosmo na kufanya makubwa kiasi katika hatua ya pili ya Ligi Daraja la Kwanza 2007, mabosi wa Azam wakamchomoa Cosmo ili akipige kwao na hawakukosea.
Akiwa Azam FC aliiisaidia klabu hiyo tajiri kupanda daraja msimu wa 2007/2008, baada ya kuifunga Majimaji FC mabao 2-0. Bao lake la kwanza katika Ligi Kuu, lilikuwa dhidi ya Toto Africans ya Mwanza. Hiyo ilikuwa Septemba 24, 2008 jijini Dar.
Pale Azam, Bocco alicheza kwa mafanikio makubwa akiisaidia klabu hiyo kutwaa makombe kadhaa kisha msimu wa 2017/2018 akatua Simba aliko hadi sasa.
MATAJI KIBAO
Achana na Kijitonyama FC alikotokea, baada tu ya Bocco kutua Azam, akaanza kujizolea mataji.
Nyota huyo ambaye kwa sasa anakipiga klabu ya Simba tayari ameshatwaa makombe matano, yakiwamo la Ligi Kuu Bara akiwa na Azam 2013/14, Ngao ya Jamii 2015/2016, Kombe la Kagame 2015, Kombe la Mapinzuzi 2016/17 na sasa ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na Simba.
NAHODHA KOTEKOTE
Sifa mojawapo ya kuwa nahodha wa timu yoyote ni nidhamu na kujituma. Hata kama kocha awe wa namna gani, pindi aonapo juhudi hizo lazima ataona umuhimu wa kukupa kitambaa cha unahodha.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Bocco. Alianza kuvaa kitambaa cha unahodha akiwa na Azam FC. Pia baada ya kutua Simba, mkongwe huyo na mfumania nyavu hodari alipewa dhamana hiyo akisaidiana na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
AWAFUNGA VIGOGO
Yuko Simba kwa sasa lakini wanamtambua vizuri tu, watani zao, Yanga nao wanamuelewa. Linapokuja suala la nani kazifunga timu zote kubwa, Bocco ndiye kinara, zote kazifunga. Kwa mujibu wa takwimu, timu hizi za Kariakoo amezifunga mara 30. Simba alioko sasa akiionea zaidi baada ya kuifunga mara 18 huku Yanga akiifunga mara 12 tu.
TIMU MBILI, JEZI MBILI
Kabla hajajiunga Simba, Bocco akiwa Azam alikuwa akitinga jezi namba 19. Hata hivyo, baada ya kutua Simba ilimlazimu kubadili namba ya jezi kutokana na namba hiyo kutumiwa na Mzamiru Yassin na sasa anavaa jezi namba 22.
MABAO KILA MSIMU
Kwenye suala la kutupia kambani, Bocco ni noma. Kwanza ndicho kilichowafanya mabosi wa Azam FC kumfungia kazi na kuhakikisha anatua Azam akitokea Cosmo. Pia Azam akatisha vile vile na sasa akiwa Simba anaendelea kutisha.
Kwa jumla Bocco ametupia zaidi ya mabao 100 tangu aanze kucheza soka lake. Mabao haya ni pamoja na 98 ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii, Kombe la Kagame, Mapinduzi, Kombe la FA na michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, hapa chini tunakuwekea mabao yake aliyofunga Ligi Kuu katika misimu yake yote aliyocheza (ukiachana na mechi ya jana kwa msimu huu wa 2018-19).
Amewahi kuwa mfungaji Bora msimu wa 2011/12 kwa kufunga mabao 19, pia ndiye mfungaji wa muda wote wa Azam na kutua kwake Simba kwa msimu mmoja ameifungia mabao 18, yakiwamo 14 ya Ligi Kuu, matatu ya michuano ya CAF na moja la Kombe la FA.
TUZO
Baadhi ya tuzo za mwezi za Ligi Kuu ni pamoja na ile ya Agosti 2016/2017 kisha ya Januari 2017/2018. Pia ana tuzo za MO zilizotolewa juzi kati tu na mdhamini wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji baada ya msimu wa 2017/2018 kumalizika. Katika tuzo hizi, Bocco alijinyakulia mbili ile ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Simba na Goli Bora.
Pia katika Ligi Kuu amewahi kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa VPL na Kikosi Bora cha VPL 2017/2018. Na katika soka la kimataifa, Bocco ameichezea Taifa Stars jumla ya mechi 56 na kuifungia mabao 14. Ameitwaa pia ubingwa wa Chalenji akiwa na Taifa Stars mwaka 2010.