Mitihani mitano ya Mzungu wa Simba

Muktasari:
Licha ya timu yake kushinda mechi tatu za awali za kirafiki, bado ana kazi kubwa kuhakikisha anapata timu bora zaidi.
KOCHA mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ana changamoto kubwa visiwani hapa, kazi yake si rahisi hata kidogo.
Licha ya timu yake kushinda mechi tatu za awali za kirafiki, bado ana kazi kubwa kuhakikisha anapata timu bora zaidi.
Simba ilicheza mechi za kirafiki dhidi ya Kombaini ya Zanzibar na kushinda 2-1, ikaifunga Braxeria 4-0 na kisha kuifunga Polisi Zanzibar mabao 2-0.
Hata hivyo licha ya matokeo hayo kuna mambo bado yanampasua kichwa kocha Kerr. Kocha huyo raia wa Uingereza pamoja na yule wa viungo, Mserbia Dusan Momcilovic, wana kibarua kizito kuhakikisha kuwa timu hiyo inakuwa bora kuliko wapinzani wao wakubwa Yanga na Azam.
Mwanaspoti ambayo imeweka kambi pamoja na timu hiyo visiwani hapa inakuletea mambo ambayo ni changamoto kubwa kwa kocha huyo pamoja na wasaidizi wake.
Uwiano wa kikosi
Kwa bahati mbaya Simba ina viungo wengi kuliko wachezaji wa idara nyingine. Timu hiyo ina viungo zaidi ya 10. Ina Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Abdi Banda, Peter Mwalyanzi, Michael Mgimwa, Awadh Juma, Mbarouk Yusuf, Simon Sserunkuma na kiungo anayejaribiwa Justice Mujabvi.
Wingi huu wa viungo unamfanya Kerr kukosa uwiano sahihi wa kikosi chake. Uchaguzi mpana alionao katika safu ya kiungo haupo katika nafasi nyingine. Hapa ana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha anapata kikosi chenye uwiano mpana.
Kusuka kombinesheni
Simba sasa ina wachezaji wengi wazuri, lakini bado wameshindwa kucheza kwa uelewano mkubwa. Hii inamaanisha kuwa Kerr ana kazi ngumu ya kusuka kombinesheni mbalimbali katika timu yake.
Kazi kubwa ya kwanza ni kutengeneza kombinesheni ya ulinzi. Kerr tayari ameanza kuwajaribu Juuko Murshid na Hassan Isihaka. Ameanza pia kuwatengeneza Abdulaziz Makame, Abdi Banda na Isihaka. Ana kazi pia ya kuwajaribu Mohammed Fakhi na Juuko. Mbali na safu ya ulinzi pia Kerr ana kibarua cha kutengeneza pacha ya kiungo na ushambuliaji. Katika ushambuliaji ameanza kuwaunganisha Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu na Elius Maguli. Licha ya wakali hao kufunga mabao manane katika mechi tatu za kirafiki, bado wameshindwa kutengeneza uelewano mzuri.
Nidhamu mchezoni
Kazi kubwa nyingine ya Kerr ni kutengeneza nidhamu ya mchezo kwa wachezaji wake. Hapa kazi ndiyo ngumu na pevu zaidi kutokana na wachezaji wengi wa Kitanzania kukosa elimu ya awali ya soka.
Nidhamu ya mchezo inapokuwa kubwa ndipo kocha anapata wigo mpana wa kuamua timu yake icheze vipi. Mfumo gani atumie na mchezaji yupi awe na majukumu fulani.
Kufunga usajili
Changamoto nyingine ya Kerr ni kuhakikisha kuwa timu hiyo inasajili wachezaji wawili makini kwa ajili ya kukamilisha kukisuka kikosi chake.
Kocha huyo tayari amebainisha kuwa anahitaji straika makini ambaye ataweza kutumia vizuri nafasi wanazozitengeneza. Kazi hii si rahisi hasa ikizingatiwa kuwa inafanyika wakati timu hiyo imemuuza Mganda Emmanuel Okwi na kuondokewa pia na Ramadhan Singano. Kazi hii pia inatakiwa kufanyika mapema ili kikosi chake kiweze kuwa na taswira halisi wiki chache kabla ya Ligi Kuu Bara kuanza.
Mechi za kirafiki
Simba imeshinda mechi zake zote tatu za kirafiki visiwani hapa, lakini ukweli unabaki palepale kwamba mechi hizo si kipimo tosha kwao. Kwenye mechi dhidi ya Polisi Zanzibar, Simba ilipigiwa shuti moja pekee langoni jambo ambalo linaashiria upinzani mdogo wa Polisi.
Mechi yao na Braxeria ambayo walishinda 4-0, Simba haikupigiwa shuti lolote langoni mwake.
Timu za Zanzibar ni laini kidogo ukilinganisha na zile za Ligi Kuu Bara. Walau mechi yao ya kesho Jumatano dhidi ya KMKM inaweza kuwa kipimo cha wastani.
Hali hii inampa Kerr changamoto kubwa katika ujenzi wa kikosi chake. Ni dhahiri kuwa atahitaji mechi ngumu zaidi za kirafiki baadaye kabla ya Ligi kuanza, japo Jumapili itaivaa SC Villa ya Uganda.