Mirambo: Kelvin ‘Mbappe’ yapo poa atarejea kikosini Serengeti Boys kama kawa

Muktasari:
- Kelvin alishindwa kuendelea na mchezo wao dhidi ya Cameroon baada ya kupata majeraha ya misuli.
Dar es Salaam.Presha ilianza kupanda kwa Watanzania baada ya mshambuliaji wa kikosi cha Serengeti Boys, Kelvin John ‘Mbappe’ kushindwa kuendelea na mchezo dhidi ya Cameroon jana.
Mashabiki wengi waliingia hofu kutokana na mchezaji huyo kuwa na uwezo mkubwa katika upande wa kushambulia kiasi cha kugeuka kuwa mshambuliaji tishio katika kikosi cha Serengeti Boys.
Hata hivyo kocha mkuu wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo aliwatuliza mashabiki baada ya kusema mchezaji wake yupo fiti licha ya kutoka nje na kushindwa kuendelea na mchezo huo.
“Anaendelea vizuri aliangaliwa na madaktari kwa ukaribu na ikaonekana ni misuli tu ndio ilimfanya ashindwe kuendelea na mchezo baada ya kukanyagwa, alipatiwa matibabu madogo ya kuondoa maumivu na hivi sasa yuko sawa,” alisema.
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Cameroon, alisema haikuwa rahisi, lakini wachezaji wake walipambana na kupata matokeo katika mchezo huo ambayo kila mmoja aliyafurahia.
Serengeti ipo nchini Rwanda ikicheza Mashindano maalumu na katika mchezo wao wa kwanza katika mashindano hayo, waliifunga Cameroon 2-1 na Alhamisi hii watacheza mechi ya pili dhidi ya wenyeji Rwanda.