Milambo anataka kitu tofauti Uturuki

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys, Oscar Milambo ameanza mikakati mahsusi kuhakikisha hawaendi kutalii Uturuki katika Mashidano ya Uefa Assits ila washindani wa kweli.
Ikiwa kambini jijini Arusha benchi la ufundi la Serenegti Boys, tayari limeanza kutafuta mechi za kirafiki na Arusha Utd na Polisi Tz kabla hawajaondoka mwanzoni mwa Machi kwenda Uturuki.
Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Milambo alisema kucheza kwao michezo hiyo kutawapa nafasi ya kuangalia utimamu wa mwili ambao wachezaji wake walionao mpaka hivi sasa.
“Zote hizi zote ni timu za Ligi Daraja la kwanza lakini lengo ni kuangalia utimamu wao, pia kuona namna gani tunaweza kucheza mchezo wa kujilinda kwa kuwa na nguvu, pia kushambulia (Combat Football) hasa tunapokutana na timu ambayo wana nguvu kuliko sisi kwenye mashindano ambayo tutakayoshiriki,” alisema.
Serengeti itaondoka nchini mapema Machi kwenda Uturuki na itarejea kutoka kwenye michuano hiyo 23 Machi kabla ya kwenda Rwanda siku mbili baadaye katika mashindano waliyoalikwa nchini humo yatakayoanza Machi 29 hadi Aprili 3 Aprili, kisha kurudi kujaindaa na fainali za Afcon U17 2019 kama timu wenyeji.