Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 10 ya kifo cha Marc-Vivien Foe

Foe akitolewa uwanjani na timu ya madaktari wa Cameroon kabla hajafariki

Muktasari:

  • Katika dakika ya 72 ya pambano hilo, huku akiwa peke yake katikati ya uwanja huo, Foe alianguka chini na kugeuza macho huku msaada wa karibu yake ukiwa wachezaji wa Colombia waliokuwa wamemzunguka wakiongozwa na nahodha, Ivan Cordoba

YOUNDE, CAMEROON

KESHO Jumatano usiku, Dunia itakuwa inaadhimisha miaka 10 kamili tangu kifo cha kushtusha cha aliyekuwa kiungo mahiri wa Cameroon na Manchester City, Marc-Vivien Foe, kilichotokea uwanjani katika pambano la Kombe la Mabara baina ya taifa lake na Colombia, tukio hilo lilitokea Ufaransa.

Ni kama ndoto, lakini tayari ni muongo mmoja tangu Foe alipofariki katika Uwanja wa Gerland unaotumiwa na klabu ya Lyon ya Ufaransa.

Kifo kilivyotokea

Katika dakika ya 72 ya pambano hilo, huku akiwa peke yake katikati ya uwanja huo, Foe alianguka chini na kugeuza macho huku msaada wa karibu yake ukiwa wachezaji wa Colombia waliokuwa wamemzunguka wakiongozwa na nahodha, Ivan Cordoba.

Baada ya jitihada za madaktari kuuamsha moyo wake ndani ya uwanja, Foe alitolewa nje kwa machela ambapo madaktari waliendelea kumhudumia kwa kumpatia hewa ya Oksijeni mdomoni. Madaktari walitumia dakika 45 kujaribu kuuamsha moyo wake na ingawa alifika katika kituo cha matibabu cha uwanja huo akiwa hai, lakini alifariki dakika chache baadaye huku madaktari wakihusisha kifo hicho na matatizo ya ghafla ya moyo.

Dunia yapata ganzi, Henry alia

Kifo cha Foe kiliishtua dunia ya wapenda soka na hata wasio mashabiki wa soka. Wengi walianza kummiminia sifa kutokana na tabia zake njema katika jamii.

Katika mechi iliyofuata usiku huohuo kati ya Ufaransa na Uturuki, Thierry Henry alionekana akilia mbele ya kamera dakika chache kabla ya pambano hilo kuanza.

Henry na wenzake pia walinyoosha vidole mbinguni baada ya Henry kufunga bao la kuongoza katika pambano hilo. Baada ya hapo, Foe alianza kupokea heshima zilizostahili ambapo ilishauriwa kwamba michuano ya Kombe la Mabara pamoja na Uwanja wa Gerland aliofia vipewe jina lake.

Kocha wa Manchester City wa wakati huo, Kevin Keegan,  alitangaza kwamba klabu hiyo isingetumia tena jezi namba 23 aliyokuwa anavaa Foe ikiwa ni heshima kwa mwanasoka huyo.

Katika uwanja wa zamani wa Manchester City, Maine Road kulitengenezwa sehemu ndogo ya kumbukumbu katika bustani ya uwanja huo kwa ajili ya kumkumbuka Foe. Katika ukuta wa korido ambalo wachezaji huwa wanatokea kuingia uwanjani, kuna maandishi yanayosomeka ‘Marc Vivien Foe – 1975–2003’.

Klabu yake ya kwanza barani Ulaya, Lens, imeupachika mtaa maarufu unaoelekea katika uwanja wao wa Felix Bollaert jina la Marc-Vivien Foe. Lens pia iliamua kuacha kuitumia jezi namba 17 ambayo Foe aliitumia kwa miaka mitano aliyoichezea klabu hiyo. Klabu ya Lyon nayo ilitangaza kutoitumia jezi namba 17 ambayo Foe alikuwa anaivaa wakati akiwa na klabu hiyo. Watu wa Lyon walionekana kuguswa zaidi na kifo cha Foe hasa baada ya kumkaribisha tena katika uwanja huo baada ya kuihama timu yao kwenda England.

Hata hivyo, baadaye Lyon walimsajili kiungo wa Cameroon, Jean II Makoun ambaye aliamua kuivaa jezi hiyo namba 17 akiwa anamkumbuka kaka yake Foe. Makoun alinukuliwa akisema: “Kwa kumbukumbu ya Marc na Cameroon yote, hiki kitakuwa kitu maalumu.”

Katika michuano ya Kombe la Mabara mwaka 2009 nchini Afrika Kusini katika Uwanja wa Loftus jijini Johannesburg, kabla ya kuanza kwa pambano kati ya Marekani na Brazil, mwanaye, Marc-Scott Foe, 14, alitoa hotuba ya huzuni kuhusu baba yake.

Azikwa mazishi ya kitaifa

Foe alizikwa Julai 8, 2003 nchini kwao Cameroon. Kabla ya kuzikwa kwake, maelfu ya Wacameroon walijipanga katika barabara mbalimbali jijini Younde kwa ajili ya kuusindikiza mwili wake.

Baadhi ya mashabiki hao walipanda katika nyumba na miti kwa ajili ya kuliona jeneza lake huku mashabiki wengi wakiwa wamevaa jezi namba 17 ambayo Foe alipendelea kuivaa.

“Alipigana kama Simba halisi, kwa ukamilifu mkubwa na aliupenda mchezo wa soka. Chochote alichopata alichangia na wengine,” alisema Askofu Joseph Akounga Essomba wakati wa Misa ya mazishi ya Foe iliyochukua saa tatu.

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Sepp Blatter, Rais wa Cameroon, Paul Biya pamoja na watu mbalimbali muhimu katika serikali na soka walihudhuria mazishi hayo.

“Hapa Wacameroon wote wameungana kwa ajili ya kumpa heshima za mwisho shujaa wa taifa aliyeanguka,” alisema mwongozaji wa shughuli hiyo kabla ya kurekebishwa na mwenzake aliyesema: “Hapana, ni dunia nzima imeungana.”

Kabla ya mwili wake kuingizwa kaburini, Foe alipewa heshima ya kuwa Kamanda wa Taifa. Wakati mwili wake ukiwa kaburini na familia yake ikiweka udongo kaburini humo, vilio vingi vilisikika. Nchini Cameroon, Foe alikuwa anasifika zaidi kwa upendo wake nje ya uwanja achilia mbali uwezo wake mkubwa ndani ya uwanja.

“Kwa miaka mitatu sasa yeye ndiye aliyekuwa ananilipia ada yangu ya shule na mahitaji yangu. Sasa ameondoka na sijui nini kitanitokea,” alisema Paul Nlib Njab, mwanafunzi aliyekuwa na umri wa miaka 14 ambaye alikuwa anatunzwa katika kituo cha watoto wasio na uwezo.

Maisha yake

Foe alizaliwa Mei 1, 1975 jijini Yaounde. Alianza kucheza soka katika klabu ya Daraja la Pili ya Union Garoua kabla ya kuhamia katika moja kati ya klabu kubwa Cameroon,  Canon Yaounde ambayo alitwaa nayo Kombe la Cameroon mwaka 1993.

Mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa ya Cameroon ilikuwa dhidi ya Mexico Septemba 1993.

Mwaka 1994 alikuwamo katika kikosi cha Cameroon kilichocheza Kombe la Dunia nchini Marekani akianza katika mechi zote tatu. Cameroon iliambulia pointi moja tu huku pia ikiambulia kichapo cha aibu cha mabao mabao 6-1 kutoka kwa Russia. Hata hivyo kiwango cha Foe kilizikosha timu nyingi kubwa barani Ulaya.

Hatimaye alisaini klabu ya RC Lens na kucheza mechi ya kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Montpellier Agosti 13, 1994. Katika misimu mitano aliyocheza Lens alitwaa ubingwa wa Ufaransa mwaka 1998.

Alitakiwa na Manchester United Mwaka 1998, akiwa ameshakubaliana maslahi binafsi na Manchester United, klabu yake ya Lens ilikataa kumuuza kwa kiasi kiduchu.

Mazungumzo yalivunjika rasmi baada ya Foe kupata nuksi ya kuvunjika mguu akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Cameroon akijiandaa na Kombe la Dunia. Foe alikosa michuano hiyo.

Atua West Ham, aweka rekodimuda mfupi baada ya kupona, Foe alijiunga na West Ham United, kwa ada ya uhamisho ya Pauni 4.2 milioni ambayo ilikuwa rekodi ya uhamisho wakati huo.

Alicheza mechi 38 akifunga bao moja dhidi ya Sheffield Wednesday. Foe pia alifunga bao katika ushindi wa 3–1 wa West Ham dhidi ya NK Osijek katika Kombe la Uefa.

Arudi Ufaransa, apata malaria

Mei 2000, Foe alirudi Ligi Kuu Ufaransa akijiunga na Lyon kwa uhamisho wa Pauni 6 milioni. Hata hivyo alikaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuugua malaria. Baada ya kupona alitwaa Kombe la Ligi mwaka 2001, na kisha ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2002.

Alikuwamo katika kikosi cha Cameroon kilichocheza fainali za Kombe la Dunia nchini Japan na Korea Kusini mwaka 2002 na alicheza mechi zote za Cameroon.

Atua Man City aweka rekodi

Msimu wa 2002-03, Lyon ilimtoa kwa mkopo kwenda Manchester City, mkopo ambao uligharimu kiasi cha Pauni 550,000. Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Leeds United ambayo walipoteza mabao 3-0.

Foe alikuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kocha, Kevin Keegan, akianza mechi 38 kati ya 41. Bao lake la kwanza klabuni hapo lilikuwa dhidi ya Sunderland katika Uwanja wa  Stadium of Light Desemba 9, 2002.

Alifunga mabao matano katika mwezi uliofuata lakini jumla alifunga mabao tisa. Bao lake la mwisho lilikuwa muhimu zaidi katika historia ya Manchester City kwa sababu lilikuwa bao la mwisho katika historia ya Uwanja wa Maine Road.

Ilikuwa ni katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sunderland Aprili 21, 2003.