Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mharami- Mashuti ya Garrincha yalinivunja mkono uwanjani

Muktasari:

Achana na marehemu Hamis Thobias Gaga aliyewahi kuchana nyavu mara kadhaa kwa makombora aliyokuwa akiyavurumishia makipa wa timu pinzani, kwa asilimia kubwa ya nyota hao wa zamani walikuwa wakifyatua mashuti ya mwendo wa Dar mpaka Moro.

ASIKWAMBIE mtu jamani nyota wa zamani wa soka nchini walijaliwa vipaji vya soka na walikuwa na nguvu na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali ya mwendo kasi.

Achana na marehemu Hamis Thobias Gaga aliyewahi kuchana nyavu mara kadhaa kwa makombora aliyokuwa akiyavurumishia makipa wa timu pinzani, kwa asilimia kubwa ya nyota hao wa zamani walikuwa wakifyatua mashuti ya mwendo wa Dar mpaka Moro.

Gibson Sembuli kwa waliomshuhudia uwanjani enzi za uhai wake akicheza wanasema alikuwa akipiga mashuti kama afyatuaye kutoka kwenye gruneti, ni sawa na ilivyokuwa kwa Makumbi Juma, Juma Mgunda, Monja Liseki, Innocent Haule na wengine.

Kama unadhani Thabani Kamusoko au Juma Abdul wanapiga mashuti makali, jua unajidanganya tu, kwani mashuti yanayopigwa na wachezaji hao ama wengine wa sasa na kusifiwa, ni cha mtoto tu kwa nyota hao wa zamani.

Ukitaka kujua namaanisha nini hebu usome mkasa uliowahi kuumpata kipa wa zamani wa Coastal Union, Simba na Taifa Stars, Mohammed Mharami ‘Shilton’ enzi akicheza ndio utajua ukweli ulivyo.

Kipa huyo aliyewahi kutamba pia na timu za Reli Morogoro kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa Msumbiji anasimulia namna alivyojikuta akivunjwa mkono akijaribu kudaka shuti la mchezaji mwenzake wa Simba.

 

ILIKUWAJE?

Anasema anakumbuka ilikuwa ni mwaka 2000 akiwa Klabu ya Simba ambapo akiwa mazoezini kwenye Uwanja wa Chuo cha Ardhi, jijini Dar es Salaam ndipo alikumbana na mkasa huo ambao anasema hatasahau.

Mharami anasema katika mazoezi hayo wakijiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara alipigiwa shuti kali na straika wa Simba aliyewahi kung’ara pia na Majimaji na Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garrincha’.

Anasema Garrincha alipofyatua mkwaju wake, hakuutilia maanani lakini wakati akijaribu kuudaka mpira huo ndipo alipojua ulikuwa na uzito gani kwani alijikuta akipata maumivu makali kabla ya kuja kubaini amevunjwa mkono.

“Mwanzoni sikuamini kama nilikuwa nimevunjika mkono, licha ya kuhisi maaumivu makali yasiyomithilika, lakini nilipokimbiziwa hospitalini kupata matibabu ndipo nikashtushwa kuambiwa nimevunjika mkono,” anasema.

“Kwa kweli tukio hilo sitaweza kulisahau, nakumbuka ilikuwa mwaka 2000, tukiwa tunafanya mazoezi Chuo cha Ardhi na Garrincha aliachia shuti hilo kali, lililouvunja mkono na kuniachia maumivu makali ambayo sikuwahi kuyasikia kabla,” anasisitiza Mharami kabla ya kuongeza;”Licha ya juhudi za kuutibu mkono huo kwa muda mrefu, ulishindikana kupona vema na kunilazimu kugoma kucheza kutokana na maumivu niliyokuwa nayapata ili nitibiwe vema kwani, hali ilikuwa tete.”

Anasema kitendo cha kugoma ili kushinikiza apatiwe matibabu zaidi tofauti ya awali aliyokuwa ameyapata, kiliwakera mashabiki wa Simba na kuona kama anayefanya makusudi na kuundiwa zengwe.

Anasema tukio hilo la shuti la Garrincha lilimuacha na kilema cha kudumu kiasi kwamba mpaka leo mkono huo wa kushoto haufanyi kazi vizuri na ndio uliomfanya astaafu soka mapema akiwa bado na uwezo wake.

 

TOTO LA ILALA

Mharami ambaye kwa sasa ni Kocha wa makipa wa timu ya taifa ya Vijana ya U17, ‘Serengeti Boys’ anasema soka alilianza tangu akiwa kinda katika mitaa ya Kariakoo- Ilala alikozaliwa, kukulia na kulicheza chandimu.

Anasema alichezea timu tofauti za Kariakoo kabla ya kuibukia kwenye Ligi Kuu (zamani Ligi Daraja la Kwanza) mwaka 1998 aliposajili wa Coastal Union ya Tanga iliyokuwa chini ya Kocha Mansour Magram.

Mharami anasema alisajiliwa Coastal ikiwa imerejea tena katika ligi hiyo iliyokuwa imeshuka miaka miwili nyuma yake. Timu hiyo ilivutiwa na uwezo wake wa kulinda vyavu.

“Nilianza kupambana kutafuta namba na baada ya mechi nne ama tano hivi ambayo Kocha Magram alinipa. Nakumbuka katika mechi hizo kuna pambano dhidi ya Mtibwa Sugar ndilo lilikuwa gumu kweli,” anasema.

Anasema mchezo ulikuwa mgumu kwa vile Mtibwa ambao walikuwa vema mno kipindi hicho ikiundwa na nyota kadhaa akiwamo Mecky Maxime, John Masamaki, Monja Liseki na wengine.

“Ninachoshukuru Mungu katika mchezo huo nilicheza vema na kudaka michomo mikali kiasi cha kocha kunimwagia sifa na kujihakikishia namba kikosini,” anasema.

 

NEEMA YAMWANGUKIA

Mharami ambaye ni mzaliwa wa Jiji la Dar es Salaam anasema aliichezea Coastal kwa misimu miwili kabla ya kuangukiwa na neema ya kusajiliwa Msimbazi mwaka 2000.

Anasema kufanya kwake vema akiwa na Coastal kuliwavutia mabosi wa timu nyingi kipindi hicho wakiwamo wa Msimbazi ambao walimshawishi ili kujiunga na timu yao na yeye hakuwa na hiyana kugomea ofa yao.

“Nilitua Simba na kuungana na makipa Doyi Moke na Miraj Juma, katika usajili wangu pia msimu huo uliwahusisha nyota wengine kama Garrincha, Amri Said na Omar Hussein kipindi hicho kocha alikuwa Nzoysaba Tauzany (marehemu kwa sasa),”anasema Mharami.

Anasema muda mfupi baada ya kutua Simba alimudu ushindani na kupata namba na mafanikio makubwa anayokumbuka akiwa na Simba kipindi hicho ni kufanikiwa kutwaa Kombe la Hedex kukata tiketi ta kucheza michuano hiyo kwa nchi ya Afrika Mashariki na kufika fainali.

“Zamani kulikuwa na michuano ya Kombe la Hedex iliyoasisiwa katikati ya 1990 nakumbuka tulikuwa mabingwa wa Tanzania wa kombe hilo na kwenda kuchuana na mabingwa wa Kenya na Uganda.”

Anasema katika michuano hiyo ya Afrika Mashariki Simba ilifanikiwa kufika fainali na kufungwa bao la jioni na ‘Majogoo’ wa SC Villa ya Uganda.

“Nakumbuka pambano hilo ndilo lililokuwa la kwanza kwangu nikiwa na Simba, pia ndilo lililokuwa pambano langu la kwanza la kimataifa kwa bahati mbaya licha ya kupambana tulipoteza mbele ya Villa,” anasema.

Unajua kama Mharami alitemwa na kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi? Unadhani sababu ilikuwa ni nini? Ungana naye Jumanne ijayo upate majibu.