Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bwalya mambo safi Pamba Jiji

BWALYA Pict

Muktasari:

  • Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa Bwalya ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, hivyo kuanzia msimu ujao ataonekana akianza kukitumikia kikosi hicho cha TP Lindanda.

UONGOZI wa Pamba Jiji umefanikisha kuinasa saini ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba raia wa Zambia, Rally Bwalya, baada ya mwanzo mwa msimu huu dili la nyota huyo kukwama katika dakika za jioni na kushindwa kukichezea kikosi hicho.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa Bwalya ameshasaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, hivyo kuanzia msimu ujao ataonekana akianza kukitumikia kikosi hicho cha TP Lindanda.

“Mazungumzo yamefikia sehemu nzuri na tayari ameshasaini mkataba huo wa mwaka mmoja, kilichobaki ni klabu na uongozi kwa sasa kumtangaza ikiona inafaa, kwa sababu tumeshamaliza msimu na malengo ya kubakia tumeyatimiza,” kilisema chanzo hicho.

Ofisa Mtendaji wa Pamba Jiji, Peter Juma Lehhet, alisema baada ya msimu kuisha na kikosi hicho kunusurika na janga la kushuka daraja, kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kufanya usajili wa nguvu, utakaoongeza tija na kuleta ushindani kwa msimu ujao.

“Suala la Bwalya naomba unipe muda vizuri wa kuzungumzia hilo kama ni kweli au laah! Ila kwa sasa tumeanza huo mchakato wa kusajili nyota wapya na kukaa chini na wale ambao mikataba yao imeisha tunaendelea na mazungumzo nao,” alisema Peter.

Bosi huyo alisema moja ya kazi kubwa aliyopewa wakati anashika wadhifa huo ilikuwa ni kuinusuru pia Pamba ili isishuke daraja na anashukuru kwa sapoti aliyoipata kutoka kwa mashabiki na viongozi wa Mkoa wa Mwanza waliofanikisha suala hilo.

Bwalya aliyetua nchini mara ya kwanza na kujiunga na Simba Agosti 15, 2020, akitokea Power Dynamos FC ya kwao Zambia, aliondoka Julai 1, 2022 akatua AmaZulu FC na baadaye Sekhukhune United FC zote za Afrika ya Kusini.

Baada ya hapo, Bwalya alirejea Zambia na kujiunga na Napsa Stars FC aliyoitumikia kuanzia Agosti 31, 2024, hadi sasa anapoachana nayo na kurejea Tanzania kuichezea Pamba iliyoanza kuiwinda saini yake tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Pamba iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imemaliza msimu ikiwa katika nafasi ya 11 kwa kuwa na pointi 34, ikishinda mechi nane, sare 10 na kupoteza 12, kati ya 30, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 33.

Kikosi hicho kilihitimisha msimu kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC FC, Juni 22, ikianza kupata bao la dakika ya 33, la nyota mshambuliaji wa timu hiyo, Mathew Momanyi, kabla ya wageni kusawazisha dakika ya 84, kupitia kwa Redemtus Mussa.