Mgunda aliamsha Simba...awataja Onyango, Kennedy

KIKOSI cha Simba kimeweka kambi ya muda Zanzibar ambapo pia itacheza mechi mbili za kirafiki ikiwamo ya leo dhidi ya Malindi kabla ya Jumanne kumalizana na Kipanga, huku kocha wa mpito, Juma Mgunda akiliamsha mapema kabla ya kuwafuata wababe wa Angola.

Kama hujui ni kwamba Simba inatarajiwa kuvaana na Primiero de Agosto ya Angola katika mechi za raundi ya kwanza, ikianza ugenini Oktoba 9, mechi itakayopigwa kuanzia saa 12:00 jioni kabla ya kurudiana nao Oktoba 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Sasa kabla ya kwenda kuvaana na de Agosto kwenye mchezo huo wa kwanza wa ugenini, Mgunda aliyeiongoza Simba kushinda mechi tatu za mashindano zikiwamo 2 za Ligi ya Mabingwa Afrika ikiing’oa Nyasa Big Bullets ya Malawi na kuilaza Tanzania Prisons katika Ligi Kuu Bara, amesema ameanza kuisoma mapema timu hiyo ili kuhakikisha wanaimaliza mapema.

Mgunda aliyetua Msimbazi akitokea Coastal Union, alisema tangu walipoona ratiba ya mechi hizo za raundi ya kwanza na kujua itavaana na wababe wa Angola aliamua kuingia chimbo na kuchukua mikanda ya video ya timu hiyo na kuanza kuisoma ambapo amebaini ni timu ya aina gani na kubadilisha mbinu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema soka ni mbinu, hivyo baada ya kuona ratiba alipata wasaa wa kuwasoma wapinzani wake ili ajue anaanzia wapi na baada ya kubaini ubora wa timu hiyo ndio maana ameamua kuitoa Simba Bara na kuipeleka visiwani Zanzibar ili kusaka kuwapa vijana wake mbinu za kiufundi za kuwakabili kwa lengo la kuvuka kuingia hatua ya makundi.

Mgunda alisema De Agosto ni timu nzuri inayohitaji utulivu, lakini akaweka wazi amepata dawa yao kutokana na kubaini kuwa timu hiyo inatumia nguvu kutokana na utimamu wao wa mwili jambo ambalo kwake anaamini mbinu alizonazo zitakuwa rahisi kwao kupenya.

“Niliwafuatilia na kuwasoma vizuri na kubaini namna wanavyocheza kazi iliyopo kwangu sasa ni kuwaandaa wachezaji wetu kimbinu zaidi ili kukwepa mitego yao,” alisema Mgunda aliyeiongoza Simba kushinda mechi tatu mfululizo za mashindano ikivuna jumla ya mabao 5-0 na kuongeza;

“De Agosto ni timu inayotumia nguvu na wachezaji wake wapo timamu hatutakuwa na ulazima wa kucheza kama wanavyocheza wao kazi iliyopo ni kuhakikisha tunaandaa kikosi ambacho kitacheza kiakili zaidi ili kukwepa kutolewa mchezoni iwapo tutaamua kwenda na staili yao.”

Mgunda alisema Simba ni wazoefu wa mashindano ya kimataifa na hata kukabiliana na figisu za nje ya uwanja na kwake kama kocha ni kuwapa mbinu na kuwajenga kisaikolojia wachezaji kwa kuwapa mechi za kujiweka fiti kabla ya kukabiliana na wababe wa Angola.

“Natambua kwa namna moja ama nyingine kuna vitu vinaweza kutengenezwa ili kuwatoa wachezaji mchezoni, lakini Simba ni timu kubwa yenye viongozi na wachezaji wenye uzoefu wa kutosha na michuano hiyo hivyo hilo kwa upande wangu silihofii na naamini tutafanya vizuri.”


AWATAJA ONYANGO, KENNEDY

Wakati huohuo Mgunda alizungumzia mabadiliko ya safu ya ulinzi kikosini hapo kuwa yanatokana na hali za wachezaji wake huku akiweka wazi kuwa kwake kila mchezaji ana nafasi ya kucheza, akiwataja Kennedy Juma na Joash Onyango ambao walicheza pamoja na Henock Inonga na Mohamed Ouattara.

“Ni kweli tangu nimeingia Simba bado sijapata kikosi cha kwanza hasa kwenye eneo la mabeki, na kama unavyojua timu huwa hazifanyi mabadiliko ya mara kwa mara kwenye eneo hilo, lakini kwangu nimelazimika kubadili kutokana na changamoto ambazo siwezi kuzikwepa,” alisema Mgunda na kuongeza;

“Mechi ya kwanza niliendeleza pale nilipoachiwa na kocha Zoran Maki kwa kuwatumia mabeki Inonga na Ouattara, lakini alipopata maumivu nililazimika kumuingiza Onyango ambaye alikuwa nje ya timu muda mrefu.”

Mgunda alisema hata kwenye eneo la pembeni pia alilazimika kubadilisha mtu kwa kumuweka nje Shomari Kapombe anayetumika zaidi na kumuingiza Israel Mwenda kwa vile alikuwa anakosa utimamu wa mwili.

“Kwa sasa kila mchezaji ana nafasi ya kucheza nawatumia kulingana na kile wanachonionyesha mazoezini kabla ya mchezo.”

Simba ikitoka visiwani itacheza mechi ya Ligi Kuu na Dodoma Jiji utakaopigwa Kwa Mkapa Oktoba 2 kabla ya kuanza safiri ya Angola.