Metacha, Sarpong kimenuka

KOCHA wa Yanga, Nesredine Nabi ametoa msimamo mkali kwa mastaa watatu wa timu hiyo akiwamo nahodha Lamine Moro ambao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za utovu wa nidhamu.

Wachezaji hao ni Metacha Mnata, Michael Sarpong na Lamine. Kuhusu Mnata na Sarpong Kocha alisema ameuagiza uongozi kuwakata sehemu ya mishahara yao na wapewe onyo kali kama watakavyofanya vivyo hivyo kwa Lamine.

Akizungumzia hatma ya cheo cha unahodha wa beki wake Lamine Moro, Nabi alisema hajafikiria kumuondoa katika nafasi hiyo ingawa anatakiwa kujitathimini juu ya kuwa mfano bora ndani na nje ya uwanja.

Nabi alisema beki huyo ataendelea na nafasi yake ya unahodha huku akimtaka kubadilika haraka ili awe nahodha ambaye atakuwa kioo kwa wengine.

“Sioni kama tutafanya uamuzi huo, Lamine alikosea na ana nafasi ya kubadilika, atabaki na nafasi yake. Kitu anachotakiwa ni kuhakikisha anabadilika ili awe mfano bora kwa anaowaongoza.

“Ukiwa kiongozi wapo ambao watakuangalia kwa kile unachofanya na ndio maana amekosea na atapewa adhabu, kuanzia hapo anatakiwa kubadilika na kuwa kiongozi wa mfano mzuri,” aliongeza.

Baada ya kuvuna pointi tisa katika mechi zake tatu za kwanza ugenini mashabiki wao wanachekelea ubora huo lakini Nabi amesisitiza kwamba bado kuna kitu anakitafuta.

Kocha ameliambia Mwanaspoti kwamba hata kama ameshinda mechi hizo tatu wala kwake sio kigezo cha kuona mambo yako sawa katika kikosi chake mpaka atakapofikia malengo yake kwa maana ya ubora wa ndani na nje ya uwanja pamoja mafanikio.

Nabi alisema bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kuendelea kufanyika ili kikosi chake kiwe katika ubora ambao anautaka uwanjani na kwamba hatua hiyo itawarudisha haraka mazoezini kuendelea na kazi.

“Ni kweli tumeshinda mechi hizo lakini hiyo sio sababu ya kuona kuna mambo yamekaa sawa, bado kuna kazi inatakiwa kufanyika kwa nguvu zaidi hapa ili tuweze kuwa katika ubora mkubwa,” alisema Nabi.

“Tunatakiwa kuendelea kuwapa vitu zaidi wachezaji ingawa hali inaridhisha wanavyopokea na kuelewa kile wanachotakiwa kufanya. Muhimu ni kuendeleza kuzingatia umakini.

“Nilisema mapema wapo wachezaji ambao wanaweza kuipa kitu kizuri timu hii endapo tutaendelea na msukumo wa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na kiu ya mafanikio,” alisema kocha huyo anayekabiliwa na mechi ya watani Julai 3.