Mechi ya kipimo cha raha!

Tuesday January 12 2021
stars 2 pic
By Ramadhan Elias

TAIFA Stars inakipiga na DR Congo jioni hii jijini Dar es Salaam. Ni mechi ya kirafiki kujiwinda na michuano ya Chan inayofanyika Januari 16 nchini Cameroon.

Kocha wa Stars, Ettiene Ndayiragije amesisitiza kwamba mechi ya leo ni kipimo halisi cha maandalizi na utayari wa Stars kuelekea fainali za Chan, huku akiomba sapoti kubwa kwa Watanzania.

stars pic

Stars ipo kambini tangu Januari 2 katika mazoezi ambayo pia Mwanaspoti limeshuhudia kwenye viwanja vya Gymkana na Benjamin Mkapa, ambapo wachezaji wameonyesha kuwa bora na wenye morali ya hali ya juu jambo ambalo linatia matumaini.

Katika mazoezi ya siku 10 yaliyokuwa yakifanyika kila siku kwenye viwanja vya Gymkana na Benjamin Mkapa yaliongezewa pia hamasa na vigogo mbalimbali wa michezo nchini waliokuwa wakipita kwa nyakati tofauti kuwapa mzuka wachezaji.

Kocha Ndayiragije amekuwa akiwapigisha tizi la maana vijana hao ikiwemo kuwaelekeza mifumo mbalimbali ambayo watakuwa wakitumia kwenye mechi watakazocheza kwenye fainali hizo.

Advertisement

Amekuwa akiwaelekeza wachezaji wake hususan washambuliaji na viungo namna tofauti ya kutengeneza mabao na kufunga, mabeki mbinu za kukaba na kuwavuruga wapinzani wao.


DHIDI YA DR CONGO

Stars ni wababe wa DR Congo kwani kwenye mechi nne za mwisho ambazo timu hizo mbili zilikutana, Stars wameshinda mbili, wakitoka sare moja na kufungwa moja.

Mechi ya mwisho ilikuwa Machi 27, 2018 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Stars walishinda kwa bao 2-0, mabao yaliyowekwa nyavuni na Mbwana Samatta dakika ya 74 na Shiza Kichuya katika dakika ya 88.

Tofauti ya michezo hiyo ni kwamba mechi nyingi timu hizo zilipokutana zimekuwa zikihusisha wachezaji wote - kwa maana ya wale wanaocheza ligi za ndani na nje, lakini mchezo wa kesho utahusisha wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara tu.

Ndayiragije ameuzungumzia mchezo huo na kueleza itakuwa mechi ambayo itawapa mwanga pia itawaonesha wapi wanapaswa kurekebisha kabla ya kuanza kwa michuano ya Chan ambapo mechi ya kwanza ya Stars huko Cameroon itakuwa dhidi ya Zambia, Januari 19.

“Hii ni mechi muhimu sana kwetu, hapo awali tulihitaji kucheza mechi mbili, lakini imeshindikana na tutacheza hii moja ambayo itatupa taswira na mwanga wa wapi tunahitaji kurekebisha na kwanini kabla ya kuanza mashindano,” alisema Ndayiragije ambaye ni kocha wa zamani wa Mbao na Azam.

Nahodha wa Stars, kipa mkongwe Juma Kaseja amesema: “Tumefanya mazoezi vizuri na kila mchezaji yupo tayari kwa mpambano dhidi ya DR Congo, utakuwa mzuri na naamini tunaweza kupata ushindi ili twende kushiriki Chan tukiwa na mzuka wa kutosha.”

Kaseja ambaye ni mchezaji wa KMC ndiye mwandamizi kikosini akiwa pia na umri mkubwa. Awali aliwahi kung’ara na Simba na Yanga.


KIKOSI

Kikosi cha sasa cha Taifa Stars chenye jumla ya wachezaji 30 unaweza kupanga timu mbili tofauti na zote zikaleta ushindani wa hali ya juu.

Mfano timu moja unaweza kuwapanga Aishi Manula, Shomari Kapombe, Edward Manyama, Ibrahim Ame, Carlos Protos, Zuberi Dabi, Deus Kaseke, Feisal Salum, Adam Adam, Rajab Athuman na Ayoub Lyanga.

Kingine wakapangwa Juma Kaseja, Israel Mwenda, Yassin Mustapha, Abdlazack Hamza, Baraka Majogoro, Said Ndemla, Yusuph Mhilu, Lucas Kikoti, Ditram Nchimbi, Farid Mussa na Paschal Gaudence.

Kwa namna mazoezi yanavyoendelea, huenda kikosi cha Stars kwenye mchezo wa majaribio leo dhidi ya DR Congo kikawa hivi:


1.Aishi Manula

2.Shomari Kapombe

3.Yassin Mustapha

4.Ibrahim Ame

5.Bakari Mwamnyeto

6.Zuberi Dabi

7.Deus Kaseke

8.Feisal Salum

9.John Bocco

10. Lucas Kikoti

11.Yusuph Mhilu.

Sambamba na hayo, mchezo huo utatumika kumuaga beki kisiki wa zamani wa Taifa Stars Aggrey Morris aliyetangaza kustaafu kuitumikia Stars siku chache baada ya kuitwa na Ndayiragije.

Advertisement