Mchawi Yanga ni huyu hapa!

Muktasari:

  • Yanga ipo Tunisia kwa ajili mchezo wa marudiano kuwania kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya, Club Africain, huku makocha Nasreddine Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze wakiingia mtegoni kulinda vibarua.

UPEPO mbaya unaendelea kuitesa na kuipeperusha Yanga katika mashindano ya kimataifa, licha ya uwekezaji mkubwa unaonekana kufanywa ndani ya timu hiyo, lakini bado imeshindwa kufuta mwenendo wa kutolewa mapema katika anga hizo.

Baada ya kuchukua mataji matatu msimu uliopita ikiwa haijafungwa hata mechi moja ya kimashindano katika Ligi Kuu ikiwa ni rekodi mpya ambayo iliingia nayo hadi msimu huu, Yanga ilijinasibu kutaka mafanikio katika mashindano ya kimataifa.

Hii ilitokana na msimu uliopita ikiwa na mzuka mkubwa na kujikuta ikitolewa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na Rivers United ya Nigeria, Yanga iliamini msimu huu jambo hilo halitokea na ilionekana kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika kikosi hicho kilianza kwa kasi kikiitupa nje Zalan FC ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, ikiifunga 4-0 mechi ya kwanza na kuifumua tena 5-0 waliporudiana mechi zote zikichezwa jijini Dar es Salaam, huku ikionekana kuwazidi mambo mengi wachovu hao.

Hatua iliyofuata Yanga ilikutana na kigingi cha Al Hilal ya Sudan yenye rekodi kubwa huku ikiwa chini na kocha mzoefu wa mechi za CAF, Florent Ibenge aliyekuwa ametoka kubeba Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na RS Berkane ya Morocco.

Katika mechi ya kwanza nyumbani ilijikuta ikilazimishwa sare ya 1-1 kabla ya kwenda kutolewa ugenini kwa kuchapwa bao 1-0 kwenye raundi ya kwanza na kuangukia play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Huko kwenye shirikisho nako hatua ya kwanza ilipigwa Jumatano ya wiki hii kwa kuanzia nyumbani na kulazimishwa suluhu na Club Africain ya Tunisia, matokeo yaliyowachefua mashabiki wa timu hiyo na kuanza kurusha lawama mbalimbali kwa timu yao kuanzia uongozi, makocha na hata wachezaji.

Mashabiki hao waliumizwa na matokeo hayo wakiona ni kama timu yao imeshatolewa kwenye michuano hiyo kwa vile itakuwa na kibarua kigumu ikielekea ugenini kupambana na Watunisia hao katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumatano ijayo nchini humo.

Ukiitazama kwa nje, Yanga ni rahisi kukuaminisha ni timu iliyostahili mafanikio kimataifa kwa aina ya uwekezaji, benchi la ufundi na hata aina ya wachezaji iliyonayo kikosini, ila kuna mambo mengi yanayodhihirisha kwamba timu hiyo haikuwa tayari kujibebesha mzigo mkubwa wa CAF.

Hapa chini ni vitu ambavyo kwa kiasi kikubwa vimechangia kuikwamisha Yanga kufikia mafanikio iliyoyatamani na hasa kutokana na mkwamo inayokutana nayo kwenye anga la kimataifa na uchambuzi huu unaonyesha ni uchawi uliopo ndani kwa ndani mwa klabu hiyo na lazima Wanayanga waukubali.

Club Africain walivyoifundisha Yanga kucheza ugenini

MAFANIKIO YA SIMBA

Huu ni mzimu unaoitesa Yanga kwa sasa kuliko inavyofikiriwa. Mafanikio makubwa ya Simba katika mechi za kimataifa, yanawafanya Wanayanga kutaka kujilinganisha nayo na kujikuta ikwamia njiani, kwa vile hata watani wao nao walifika hapo kwa kutokwa jasho na damu kwa muda mrefu.

Misimu mitano ya michuano ya CAF kwa kufika hatua ya makundi mara tatu, zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika, ndicho kitu kinachoitesa Yanga na kuamini hata timu yao ina uwezo wa kufika hapo kirahisi na mwishowe kuishi kwa presha kubwa.

Simba ilifika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2018-2019 na kuvuka hadi robo fainali kama ilivyokuwa 2020-2021 ilipotinga makundi pia na kuvuka hadi robo fainali na msimu uliopita ilikwama Ligi ya Mabingwa lakini ikatinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufika tena hadi robo fainali.

Yanga inasahau katika misimu hiyo mitano, Simba ilikwamia raundi ya awali msimu wa 2019-2020 na raundi ya pili msimu wa 2021-2022 kwa Ligi ya Mabingwa na raundi ya kwanza 2018 katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama Yanga haitabadilisha mtazamo na kuijenga timu kama ilivyofanya Simba na kufika ilipofikia, huenda ikasumbuka zaidi na kuishi kwa presha kubwa itakayowatesa makocha, wachezaji na hata viongozi na kushindwa kujipanga vizuri.


HAKUNA UMOJA

Kitu kingine kinachoitesa Yanga kwa sasa ni kukosa umoja wa dhati. Hakuna siri, ni lazima Yanga irudi chini na kujiuliza kipi kinakwamisha umoja ndani ya klabu yao, bahati mbaya ni vigumu kwa viongozi wao kusema lakini kuna vigogo baadhi waligoma kushirikiana na utawala wa Injinia Hersi Said katika kuisimamia timu hiyo.

Haina maana kwamba Hersi hakuwaita watu hao na kutaka kushirikiana nao, alifanya hivyo lakini baadhi walikataa kujiunga naye moja kwa moja. Hili ni lazima watu wazito zaidi hasa waliopo katika Baraza la Wadhamini wakae chini na pande zote za utawala wa Hersi kisha watafute suluhu warudi kuunganisha nguvu.

Nyuma ya pazia wanachama na mashabiki wa Yanga wanajua viongozi wao wanashirikiana na wana umoja wa nguvu, lakini hali halisi haipo hivyo. Wapo ambao wameamua kukaa pembeni wakati klabu inamhitaji mwenye nguvu ndogo na kubwa kuunganisha kwa pamoja kuhakikisha mafanikio yatakuja.


KOSA LA USAJILI

Baada ya kuchukua mataji matatu Yanga ilifanya usajili kwenye dirisha kubwa wakilenga kuleta watu ambao wangekuja kuunganisha nguvu na wale waliowakuta kutengeneza timu kamili yenye ujazo wa kushindana kimataifa.

Yanga iliwasajili beki, Joyce Lomalisa, viungo, Gael Bigirimana, Bernard Morrison, Stephane Aziz KI, winga Tuisila Kisinda aliyeingia kwa mkopo akija kuchukua nafasi ya mshambuliaji Lazarous Kambole ambaye naye aliingia katika dirisha hilohilo na kutolewa dirisha hilohilo.

Ukiangalia kwa mapana usajili wa wachezaji hao utaona ni Aziz KI na pengine Morrison ndio pekee ambao walifanikiwa kuonyesha uwezo huku wengine hawana kitu cha kuiongezea Yanga.

Baada ya kupata shida katika beki ya kushoto ujio wa Lomalisa ukaendelea kuitesa Yanga kwa beki huyo Mkongomani kushindwa hata kumpiku kiraka Farid Mussa ambaye alikuwa anaziba tu nafasi hiyo.

Badala yake beki mzawa, Kibwana Shomari akionekane ndiye mbadala wa Lomalisa ambaye aliendelea kula fedha za bure akiwa benchi huku Kibwana akiwa kiraka wa beki wa kulia Djuma Shaban.

Kumbuka Lomalisa aliletwa baada ya David Brayson aliyesajiliwa msimu uliopita kusumbuliwa na majeraha ya kila mara na kushindwa kuibeba timu.

Bigirimana naye licha ya kushushiwa sifa nyingi wakati alipofika lakini alionekana ni kiungo ambaye umri umekwenda na kushindwa kuleta kile ambacho kilitarajiwa na kubaki kuwa mhamasishaji akiwa katika benchi badala ya kuwaongoza wenzake uwanjani.

Hii ilithibitisha Yanga bado haikuwa na kitu kikubwa cha ziada katika usajili ambao waliufanya. Swali la kujiuliza ni namna gani wanashirikiana katika kujiridhisha juu ya aina ya wachezaji ambao wanawasajili?

Yanga lazima irudi chini na kujitathimini katika eneo hili la usajili ingawaje inajulikana sio kila wakati utapatia katika usajili lakini itoshe kuonyesha kwamba tatizo hilo lilichangia kuwapa shida katika safari yao ya kimataifa.

TOFAUTI YA MAKOCHA

Wakiwa safarini Sudan, Yanga ilikumbana na mgogoro wa makocha wake wawili, kocha mkuu, Nasreddine Nabi na msaidizi wake, Cedric Kaze ambao walishindwa kuiva chungu kimoja.

Shida hapa ilianzia katika ujio wa Kaze, ikumbukwe kocha huyo alikuwa Yanga kabla kutimuliwa Machi 7, 2021 baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha dhidi ya Coastal Union na baadaye kutoa sare na Polisi Tanzania jijini Arusha.

Baada ya kuondoka Kaze aliletwa Nabi akiipokea timu kutoka kwa aliyekuwa kocha wa muda mzawa Juma Mwambusi na raia huyo wa Tunisia akaanza vyema kazi yake na kumaliza nafasi ya pili msimu huo.

Msimu mpya ulipokuja akaletewa Kaze kama kocha msaidizi hii haikuwa sawa, kwani ilihitaji weledi wa Mrundi huyo kutambua nafasi yake kutokana na kwamba alikuwa hapo kama kocha mkuu ni rahisi kuvurugana kwa kuwa aliondolewa wakati alikuwa akitamani kuendelea kuwepo anga hizo.

Baadaye makocha hao wakaanza kupishana hadharani hali ambayo ilizorotesha ustawi wa timu yao, hali ambayo msimu huu ilishamiri zaidi na kutumika muda mwingi kutunishiana misuli.

Viongozi wa Yanga walichelewa kuliona hili na walipaswa kulishughulikia haraka na kuwaonyesha tofauti zao na kumpa kocha mkuu nafasi yake ya msingi ya kuchagua msaidizi wake kama ambavyo utaratibu unavyotaka.


HATA SIMBA ILIWAKUTA

Mgogoro kama huu uliwahi pia kuikumba Simba, lakini uliwahiwa kutatuliwa mapema baada ya Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems akiwa na Mrundi, Masoud Djuma. Makocha hao walizinguana kwa kushindwa kuwa pamoja katika kazi zao na kuanza kuiathiri Simba.

Viongozi wa Simba waliliona kwa haraka na kufanya uamuzi mzito kumuondoa Djuma na kumtaka Aussems kutafuta msaidizi wake na kuletwa mzawa Denis Kitambi na baadaye Suleiman Matola mpaka pale Mbelgiji huyo alipoonekana naye kushindwa na kuondolewa.

UBORA NA MAKUNDI KWA MASTAA

Mgogoro wa makocha hao wa Yanga ulizalisha makundi ndani ya kikosi hicho, wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi ya kucheza walikimbilia upande wa Kaze na wengine kukaa upande wa Nabi. Mgogoro ambao ulikuwa unaendelea kuitafuna Yanga ndani kwa ndani.

Viongozi wa Yanga nao wakawa na tathimini yao wakiona timu chini ya Nabi ni kama imepungua ubora wakidai kuwa hata muda wa mazoezi umepungua kutokana na muda mrefu kutumika katika kusigana kwa makocha hao.

Wachezaji wakaanza kuonekana wa kawaida kutokana na kushindwa kupata mazoezi ya kutosha hali ambayo ilizidi kuwagawa viongozi wa timu hiyo na Nabi ambaye alikuwa akipingana na hoja hizo za viongozi wa Yanga.

Yapo madai kwamba wachezaji wamegawanyika katika makundi kutokana na namna usajili wao ulivyofanywa na hata wanavyochukuliwa kikosini na wapo waliojitengenezea mamlaka zao wenyewe na kuchangia kuwapa ugumu makocha hasa katika kudhibiti suala la nidhamu kambini.


MADENI YA WACHEZAJI

Hivi karibuni kukaibuka madai mengine kuwa lipo kundi la wachezaji linadai ada za usajili baada ya kuongeza mikataba mipya wakiwemo mastaa wakubwa ambao nao baada ya kuonekana ahadi wanazopewa hazitimii walianzisha migomo baridi wakikosa hata vipindi vya mazoezi na hata kwenda kwenye mechi bila morali ya kutosha.

Hali kama hiyo hupunguza morali ya wachezaji na wakati mwingine kushindwa kujitoa uwanjani na kuiangusha timu na mwishowe lawama zinawaendea makocha ilihali waliosababisha hali hiyo ni viongozi wa kushindwa kuheshima makubaliano na wachezaji na pia kuwa wa kweli mbele yao.


NINI KIFANYIKE

Yanga itolewe au isitolewe dhidi ya Club Africain lakini viongozi wanapaswa kujitathimini na mfadhili wa klabu hiyo anapaswa kukaa mezani na baraza la wadhamini kuangalia upya uti wa mgongo wa klabu hiyo kiuongozi na mambo yanavyokwenda kisha kujisahihisha kabla hawajapotea zaidi.

Bahati kubwa katika baraza lao la wadhamini lina watu wazito wenye akili ya soka na utawala wakiwepo pia viongozi wa serikalini, wanatakiwa pia kukaa chini na Kamati ya Mashindano ambayo ni wazi itakuwa inajua wapi kunavuja na baadaye kufanya kikao jumuishi kitakachokwenda kutoa dira njema ya utawala wa Rais Hersi Said.

Kitu kingine kinachopaswa kufanywa kwa sasa ni kuhakikisha inawaondoa makocha wote, yaani Nabi na Kaze katika nafasi zao ili wapishe akili mpya.

Inawezekana wapo ambao wanaona uwezo wa makocha hao umefika mwisho hasa kutokana na mechi za kimataifa, lakini katika kujenga ustawi mpya katika vyumba vya wachezaji ni bora ikaja sauti mpya kurudisha morali kwa wachezaji ambao baadhi yao ni kama wamejikatia tamaa.

Ni lazima Yanga itumie dirisha dogo kupunguza wachezaji ambao wameshindwa kuibeba timu na kuleta wengine wenye viwango vya kuisaidia katika michuano ya ndani na ya kimataifa na wale watakaowabakisha ni lazima wajengwe kisaikolojia na kuwafanya wawe pamoja kwa ajili ya timu.