Mbwembwe za mechi ya watani

MECHI ya watani wa jadi, Simba na Yanga, itabaki kuwa ya kipekee kutokana na mambo yanayofanyika kabla ya mchezo na hata baada, pia kwa namna inavyokuwa na presha kuanzia kwa viongozi mpaka mashabiki wa klabu hizo.
Mwanaspoti linakuletea mifano halisi inayothibitisha upekee wa mechi hiyo, tofauti na wanavyokutana na klabu nyingine kama Kagera Sugar, Stand United, Mbeya City, Prisons na nyinginezo.
Kwanza, sababu kuu inayofanya mechi hiyo iwe ya kipekee ni kwa vile klabu hizo zilishiriki kwenye harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, 1961.
Simba na Yanga zilitumika katika harakati hizo baada ya Wakoloni kukataza wananchi kukaa makundi makundi, ndipo walitumia fursa ya timu hizo kufanya shughuli za kisiasa na kwa kiasi kikubwa ilisaidia harakati za kupata uhuru.
Ukiachana na sababu hiyo, pia kuna mambo yanayotokea kipindi cha maandalizi ya mchezo huo ambayo husababisha mchezo kuwa na presha ya juu.
USHIRIKINA/ULINZI
Mechi ya watani hao wa jadi inakuwa na vituko vya aina yake, makomandoo wa klabu hizo wanaweka ulinzi mkali kwa wachezaji wanapokuwa wanaingia uwanjani hadi kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo.
Ulinzi wake si masihara ambapo mtu wa Yanga kabla ya mechi haruhusiwi kusogelea eneo la Simba, vivyo hivyo mtu wa Simba haruhusiwi kugusa eneo la Yanga. Ukisogea tu, makonde yatakuhusu.
Ishu ya pili ni imani za kishirikina. Straika wa zamani wa Simba na kisha Yanga, Said Maulidi ‘SMG’ amewahi kuliambia Mwanaspoti akisema: “Nimevishuhudia vitu hivyo katika klabu hizo, ila sikuviamini. Nilichokuwa nakifanya ni kujituma kwa bidii kuanzia mazoezini mpaka uwanjani, nilifanikiwa kwa njia hiyo na si ushirikina ambao unategemeana na imani ya mtu mwenyewe.”
POSHO KIBAO
Kama kuna wakati wachezaji wa timu hizo huneemeka, basi ni wanapokutana kwenye mechi ya watani kama hii ya leo Jumamosi. Posho inakuwa nono tofauti na wanapocheza na timu nyingine.
Mfano kwa Simba, katika mechi zao za kawaida posho inayotolewa kwa wachezaji ni Sh10 milioni pindi wanaposhinda, lakini inapofika wakati wa mechi hiyo ya watani posho hiyo hupanda hadi Sh40 milioni.
Vivyo hivyo kwa Yanga, wachezaji wanapewa posho nono za kuwahamasisha.
KAMBI ZAO
Kwa kawaida nje ya mechi ya watani, kambi zao zinawekwa jijini Dar es Salaam ambako ndiko makao makuu ya klabu hizo yalipo, ila ifikapo wakati wa mechi baina yao utasikia Simba, wameenda Zanzibar na Yanga, Morogoro au vinginevyo.
Kambi hizo hutumia gharama kubwa kuhakikisha wachezaji wanakaa hoteli za kifahari, wanapata msosi wa nguvu na mazingira mazuri ya maandalizi. Pia kambi hizo za mbali hulenga kuwalinda wachezaji wao wasirubuniwe na wapinzani.
Staa wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amewahi kukaririwa na Mwanaspoti akisema ulipofika wakati wa mechi hizo, walilindwa kama lulu.
“Yaani ilikuwa ngumu hata kwenda dukani, ukihitaji kitu chochote anaenda mlinzi kukununulia kwa sababu ya presha ya hali ya juu, inayotokana na tambo za mashabiki mtaani,” alisema.
MALIPO/MADENI
Ikifikia wakati wa mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, wachezaji wanalipwa madai yao yote wanayokuwa wanaidai klabu, ili wasiingie uwanjani na mawazo wakashindwa kutimiza majukumu yao. Kama kuna mchezaji anadai fedha za usajili atalipwa. Kama kuna anayedai mishahara atalipwa. Hakuna anayeachwa na deni ili asipate kisingizio uwanjani. Kama hatalipwa basi ataahidiwa kuwa malipo yake yatapatikana kutokana na mapato ya mchezo huo.
VIKAO KIBAO
Kuelekea mechi ya watani, vikao vya mabosi na matajiri wa timu hizo huwa vingi kupindukia. Matajiri hao pamoja na viongozi wa kisiasa, hutembelea kambi za timu hizo na kuzungumza na wachezaji.
Makocha na viongozi wa klabu pia hufanya vikao vya mara kwa mara na wachezaji ili kumfunga mtani. Kazi ipo.