Mbrazil afichua siri, aigeukia Azam

Muktasari:

  • Simba ilifungwa mabao 3-0 na Raja kwenye mechi ya Kundi C na kujikuta ikishuka hadi mkiani mwa kundi hilo ikiwa haina pointi wala bao na kocha Robertinho alisema kilichotokea ni sehemu ya mchezo kwani walicheza na timu kubwa, lakini wanajipanga kwa mechi zilizosalia.

KIKOSI cha Simba juzi kilipoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Raja Casablanca na kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' akifichua kilichowaponza, lakini akawa moyo mashabiki kwamba kazi haijaisha ila kwa sasa anamalizana kwanza na Azam FC.

Simba ilifungwa mabao 3-0 na Raja kwenye mechi ya Kundi C na kujikuta ikishuka hadi mkiani mwa kundi hilo ikiwa haina pointi wala bao na kocha Robertinho alisema kilichotokea ni sehemu ya mchezo kwani walicheza na timu kubwa, lakini wanajipanga kwa mechi zilizosalia.

Kocha huyo, aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa  kujitolea kwenye mechi ya juzi, ila anatamani kupata muda zaidi wa kuitengeneza timu kwani tangu ameanza kazi si muda mrefu.
Robertinho alisema ukiangalia Raja kuna wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya CAF, wamekaa kwenye timu kwa pamoja kwa muda mrefu hadi kuwa na kikosi bora kama alichokuwa nacho kwa wakati huu.

Alisema ila yote hayo yamepita yale makosa wamejifunza na watakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye mechi nne zilizosalia ikiwamo ya wiki hii dhidi ya Vipers ya Uganda itakayopigwa ugenini.

"Kulingana na hali yetu ilivyo kwenye kundi tunahitaji nasi kwenda kuweka rekodi pale Uganda kushinda dhidi ya Vipers ili kurudisha hali na morali kwa wachezaji na mashabiki kwenye mchezo wa marudiano hapa nyumbani," alisema Robertinho na kuongeza;
"Kama tukifanikiwa kupata ushindi na Vipers malengo yetu ya kufuzu hatua hii yatakuwa kwenye hali nzuri, kama ambavyo tuatashinda mechi ya Azam hali na morali kwa wachezaji itarudi na tutaendelea kupunguza umbali wa pointi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara."

Katika kuhakikisha hataki utani, kocha kutoka Brazili aliamua kuwaitia wachezaji wote kambini ili kujifua kwa mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa, kisha kuendelea kujifua kwa mchezo wa ugenini dhidi ya Vipers ya Uganda.

Wachezaji wa timu hiyo waliingia kambini jana jioni kuiweka miili sawa baada ya mchezo mgumu wa michuano ya CAF na Robertinho alisema hakuna muda wa kupoteza, kutokana na kubanwa na ratiba ngumu waliyonayo ya kucheza mechi mbili ndani ya siku sita.

Robertinho alisema ndani ya siku mbili hizi nguvu, akili na maandalizi ingawa kuna muda mchache kwa mchezo wa Azam, ambao wanahitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri.

Alisema matokeo ya mechi dhidi ya Raja kupoteza nyumbani tofauti na matumaini waliyokuwa nayo yaumiza kila mmoja, lakini ni lazima wasahau ili kujipanga kwa mechi zilizopo mbele yao kuhakikisha wanatimiza malengo kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF.

"Ukiangalia kimahesabu bado hatujapoteza nafasi ya kufuzu robo fainali, hilo linawezekana kama tutafanya vizuri kwa kushinda mechi nne zilizobaki kwenye kundi hilo. Bado tuna nafasi licha ya kuanza vibaya," alisema Robertinho na kuongeza;
"Nitazungumza na wachezaji kila mmoja kwa nafasi yake tuna kazi kubwa ya kufanya na kujitolea kuliko kawaida kulingana na majukumu yetu ili tuweze kwenda robo fainali kama malengo yetu yalivyo.

"Mechi inayofuata na Azam, wenzetu wamepata muda wa kutosha wa kujiandaa na kupomzika hilo kwetu halipo ila kwa namna yoyote wachezaji wangu wanatakuwa kujitolea na kuhakikisha ushindi unapatikana."

Robertinho alisema mechi ya duru la kwanza, Simba ilipoteza ikitoka kucheza na Yanga na safari hii inakutana na Azam ikitoka kucheza mechi ngumu ya CAF, ila ni lazima wapambane ili kupata matokeo kabla ya kugeukia mechi na Vipers.