Mbeya City yabanwa Nyamagana

Tuesday October 12 2021
mbeya pic

Wachezaji wa Mbeya City (fulana Nyeupe) wakimenyana na wachezaji wa Copco Veteran (fulana ya bluu) ya jijini Mwanza katika mchezo wa kirafiki uliopigwa uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Timu hizo zimetoka suluhu ya 0-0. PICHA NA MGONGO KAITIRA

By Damian Masyenene

KIKOSI cha Mbeya City kimeshindwa kutamba mbele ya Copco Veterani baada ya kulazimishwa suluhu ya 0-0 katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mchezo huo umepigwa leo saa 8 mchana ambapo timu zote mbili zimeutumia kujipima kwa mechi zao zijazo mwishoni mwa wiki, ambapo Mbeya City watavaana na Kagera Sugar Oktoba 16, huku Copco Veterani wakiwakabili Nyaishozi  Oktoba 17 katika Dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Katika mchezo huo kila timu ilipambana kutengeneza nafasi za kufunga magoli bila mafanikio huku safu za ulinzi na magolikipa wakitimiza kwa usahihi majukumu yao ya kuzuia michomo isiguse nyavu zao.

Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Mathias Wandiba amesema wameamua kucheza Nyamagana saa nane mchana ili kupata uzoefu na kuzoea mazingira kwani mchezo wao na Kagera Sugar utapigwa muda kama huo huku akitamba kuwa wamedhamiria kuvuna pointi zote tisa za Kanda ya Ziwa.

Kocha Mkuu wa Copco Veterani, Daddy Gilbert amesema anafarijika na ubora wa kikosi ambacho kimezidi kuimarika kiufundi na muunganiko, ambapo amesisitiza malengo ni kupanda daraja na ikishindikana wasalie kwenye ligi hiyo.

Mbeya City inaanza mechi za ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold baada ya kuanzia nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons wakishinda 1-0 na sare ya 2-2 na Mbeya Kwanza wakivuna pointi nne katika mechi zao mbili za Ligi Kuu.

Advertisement

Copco Veterani ya Mwanza katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (zamani Daraja la Pili) msimu huu imepangwa kundi B pamoja na timu za Mbuni na Arusha FC (Arusha), Mbao na Alliance (Mwanza), Nyaishozi (Kagera), Kurugenzi (Simiyu) na Rhino Rangers ya Tabora.

Advertisement