Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeya City waipeleka Kagera Sugar ilipofia Simba

Mbeya. Baada ya kutumia zaidi ya masaa matatu kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar, Mbeya City imefichua kilichowaangusha katika mechi zake tatu za nyuma, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mathias Lule akisema amepata dawa.

City ilikuwa na matokeo mazuri ikiwamo kuzisimamisha timu kubwa, Simba, Yanga na Azam kwa kuvuna jumla ya pointi tano kwa miamba hao wa soka nchini lakini kwa sasa kasi yao imeonekana kupungua haswa kufululiza sare nyingi.

Timu hiyo ya jijini hapa mara ya mwisho kushinda mechi yake ilikuwa Januari 20 ilipoinyuka Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye uwanja wa Sokoine na tangu hapo imekuwa ni sare na kupoteza.

Katika mechi nne za mwisho, timu hiyo imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Namungo mabao 2-0 kisha suluhu dhidi ya Yanga sawa na Mbeya Kwanza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika mechi hizo, timu hiyo ilikuwa ikijifua kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga,huku matokeo ya ushindi ikiwamo Simba walipoichakaza bao 1-0 walikuwa wameweka kambi viwanja vya Isyesye ambapo sasa wamerudi tena kujiwinda dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumza baada ya mazoezi ya leo Jumatano yaliyofanyika kwenye uwanja wa Isyesye, Lule amesema kukosa ushindi kwenye mechi zilizopita ni kutokana na uwanja waliokuwa wanatumia wa Shule ya Sekondari Iyunga na kwamba kwa sasa wamerejea Isyesye, hivyo mchezo na Kagera Sugar watashinda.

Pia amesema anafahamu mchezo huo utakuwa mgumu lakini kutokana na ukame waliopitia hawatakuwa na mzaha katika kupata alama tatu na kurudi kwenye nafasi nzuri.

"Tumeamua kurudi hapa uwanja wa Isyesye kuhakikisha mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar tunashinda, tulipokuwa hali haikuwa nzuri tunataka ushindi Jumamosi na kukaa nafasi nzuri, vijana wako fiti kila mmoja ana ari na morari kubwa," amesema Lule.

Timu hizo zinakutana ikiwa Mbeya City wamekusanya pointi 25 nafasi ya tano, huku Kagera Sugar wakiwa na alama 21 nafasi ya tisa baada ya pande zote kucheza mechi 17.