Mbeya City kufumua kikosi

Muktasari:
- Mbeya City imerejea Ligi Kuu baada ya kukosa uhondo huo misimu miwili mfululizo na msimu huu imemaliza nafasi ya pili Ligi ya Championship na pointi 68 nyuma ya vinara na mabingwa, Mtibwa Sugar waliovuna 71.
WAKATI Mbeya City ikiendelea kuchekelea kurejea Ligi Kuu Bara, uongozi wa timu hiyo umesema pamoja na kazi nzuri waliyofanya wachezaji na benchi la ufundi, lakini mabadiliko na maboresho hayaepukiki kwa ajili ya msimu ujao.
Mbeya City imerejea Ligi Kuu baada ya kukosa uhondo huo misimu miwili mfululizo na msimu huu imemaliza nafasi ya pili Ligi ya Championship na pointi 68 nyuma ya vinara na mabingwa, Mtibwa Sugar waliovuna 71.
Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ilianza msimu chini ya Kocha Salum Mayanga aliyehudumu kwa zaidi ya msimu mmoja, mechi sita za mwisho ilimpa kibarua Malale Hamsini na kupanda Ligi Kuu.
Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema baada ya kutimiza malengo, wanawashukuru wadau, mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi nzuri na sasa mipango inaanza haraka kusuka kikosi.
Alisema mabadiliko na maboresho lazima yawepo kwani wanaingia kwenye ligi tofauti yenye kutaka ubora ili kuleta ushindani.
“Kwanza kuna ambao wanaweza kupata ofa kubwa hatuwezi kuzuia akiwamo kocha, hivyo sisi tutaangalia mahitaji yetu kuhakikisha tunaendana na matakwa ya sehemu tulipo.
“Japokuwa uongozi utajitahidi kuwabakisha wale walioonyesha zaidi kiwango ili msimu ujao tuendelee nao, tutakuwa na maandalizi ya mapema ili kuendeleza historia yetu ya ushindani,” alisema Nnunduma.
Kuhusu siri ya mafanikio, kiongozi huyo ambaye ni mchumi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, alisema ushirikiano wa ndani na nje ya uwanja ndicho kilichowapa matokeo mazuri.
Alisema kama alivyoahidi wakati akikabidhiwa timu ataipeleka kwa wananchi, ndiyo kilichangiza zaidi kwa City kufanya vizuri msimu huu.
“Tuliamua kuwapa wananchi timu yao, tumeshirikiana kwa muda wote na timu itakuwa kwao muda wote, sisi tunabaki kwenye utekelezaji, tunaamini tutakuwa bora hata msimu ujao,” alisema kigogo huyo.