Mbeya City haipoi yaua Sokoine

Muktasari:

  • Mchezo huo ulikuwa wa kirafiki, ambapo Mbeya City wanajipanga kuwakaribisha KMC, huku Itezi wakiwasubiri ndugu zao, Ilemi katika mchezo wa kombe la Azam shirikisho (ASFC).

Mbeya. Mziki wa Mbeya City hauzimiki, kwani baada ya kucheza mechi sita bila kupoteza, leo kikosi hicho kimejipima nguvu dhidi ya Itezi FC na kuwanyuka mabao  3-1.

Mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa ulikuwa wa kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC utakaopigwa Jumamosi ya wiki hii kwa raundi ya saba.

Mbeya City walio nafasi ya nne kwa pointi 10 ni miongoni mwa timu tatu ambazo hazijapoteza mechi hata moja msimu huu ikiwa ni vinara Yanga wenye alama 16 na Simba pointi 14.

Kwa upande wa Itezi wameutumia mchezo huo kujiweka sawa na mechi yao ya kombe la shirikisho (ASFC) dhidi ya Ilemi mechi ambayo itapigwa Alhamisi ya wiki hii.

Katika mtanange huo licha ya pande zote kuonesha soka safi, lakini Mbeya City ndio walitakata zaidi na kuweza kuibuka na ushindi huo.

Mabao ya Gasper Mwaipas dakika ya 16, Eliud Ambokile dakika ya 33 na Edgar Mbembela dakika ya 40 yalitosha kuwamaliza wapinzani walioambulia bao moja kupitia kwa Benson Raphael dakika ya 45.