Mayele arejea kikosini, Yanga ikijifua Sokone

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mayele hakuwepo kwenye kikosi kilichocheza jana Jumanne dhidi ya Mbeya City na sasa amerejea kikosini na leo amejifua pamoja na mastaa wengine, huku Diarra naye akiwa amewasili jijini Mbeya tayari kwa mechi yao ya kufunga msimu dhidi ya Tanzania Prisons na kukabidhiwa kombe.

Baada ya kukosekana katika mchezo wa jana dhidi ya Mbeya City, Straika wa Yanga Fiston Mayele ametua jijini Mbeya kuungana na timu yake kwa ajili ya mchezo ujao na Tanzania Prisons.

Mayele hakuwepo kabisa katika kikosi cha timu hiyo wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City walipoambulia sare ya mabao 3-3 huku Yanga ikitoka nyuma na kusawazisha yote kupitia kwa Bernard Morrison (mawili) na Salum Aboubabakari 'Sure Boy'.

Leo katika mazoezi ya Yanga yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine kinara huyo wa mabao kwenye Ligi Kuu (16) alikuwa kikosini sambamba na mastaa wengine huku ikielezwa kuwa hata kipa wao Djigui Diarra tayari ametua jijini hapa kuungana na wenzake.

Kurejea kwa Mayele ambaye ametoka kuchukua tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika alipofunga mabao saba, inarejesha furaha kwa mashabiki wake na Yanga kwa ujumla kwenye vita ya ufungaji bora ligi kuu.

Straika huyo raia wa DR Congo kwa sasa yupo kwenye vita kali ya kuwania kiatu cha mfungaji bora dhidi ya nyota wa Simba, Saido Ntibazonkiza ambaye jana aliweka rekodi ya kwanza kufunga hatitriki mbili Ligi Kuu na kufikisha mabao 15 akizidiwa moja tu.

Ntibazonkiza aliyewahi kucheza Yanga na Geita Gold alitupia mabao matano peke yake wakati Simba ikiisambaratisha Polisi Tanzania mabao 6-1 na kuwashusha daraja Maafande hao.